Polisi Tanzania,Pamba zang'ara Ligi ya NBC Championship

KILIMANJARO-Polisi Tanzania imepata ushindi wa kwanza kwenye Ligi ya NBC Championship dhidi ya Ruvu Shooting kwa bao 1-0.

Ushindi huo ulihakikishwa mapema dakika ya 15 kwa bao la Denis Mushi na kufanya Ruvu Shooting kupoteza mchezo wa pili mfululizo baada ya kufungwa dhidi ya FGA Talents mabao 2-1 katika mchezo wa ufunguzi.

Pamba ya Mwanza imeendeleza makali yake kwenye Ligi ya Championship baada ya leo kupata ushindi wa pili mfululizo kwa kuifunga Pan African ya jijini Dar es Salaam bao 1-0.

Bao pekee la Pamba katika mchezo huo likifungwa na Jamal Mtegeta kwa mkwaju wa penalti dakika ya 80.

Bao hilo ni la pili mfululizo kwa Jamal Mtegeta aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji, ambapo bao lingine alilifunga katika mchezo uliopita dhidi ya Cosmopolitan na Pamba ilishinda kwa mabao 4-0.

Ushindi huo unaifanya Pamba, kujichimbia kileleni mwa ligi hiyo ikivuna pointi sita huku ikiwa haijaruhusu bao, wakati Pan African inarejea Dar es Salaam na pointi tatu ilizozivuna kwenye ushindi wa mabao 3-2 mbele ya Copco FC.
 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news