TARURA:Bilioni 50/- kunufaisha wananchi mkoani Iringa

IRINGA-Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji wa Barabara za Vijijini kwa Ushirikishaji na Ufunguaji wa Fursa za Kijamii na Kiuchumi (Roads to Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE).
Ni katika Mkoa wa Iringa lengo likiwa ni kujenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilomita 33 ili wananchi waweze kuzifikia huduma za kijamii kwa urahisi pamoja na kusafirisha mazao kwenda sokoni.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor H. Seff wakati wa ziara ya Kamati ya Ufundi ya Mradi wa RISE ilipofanya ukaguzi wa ujenzi wa barabara ya Wenda–Mgama yenye urefu wa kilomita 19 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Sambamba na ujenzi wa barabara ya Mtili–Ifwagi yenye urefu wa kilomita 14 iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambapo zote zinajengwa kwa kiwango cha lami na tayari wakandarasi wote wamefika eneo la kazi, ambapo hatua za awali za utekelezaji zimeanza.
‘’Leo nimefanya ukaguzi wa mradi wa RISE nikiwa nimeambatana na Kamati ya Ufundi ya mradi na lengo kuu hasa ni kuhakikisha mpango uliowekwa kati ya TARURA na wakandarasi wanaotekeleza mradi huo wanatekeleza kama ilivyopangwa.
"Na kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kulingana na mkataba na kama kuna changamoto yoyote ifahamike na kutatuliwa kwa wakati ili miradi yote ikamilike mapema na kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,"amesema Mhandisi Seff.
Aidha, Mhandisi Seff amemuagiza Meneja wa TARURA Mkoa wa Iringa kuhakikisha anasimamia kwa karibu mikataba ya mradi huo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mahitaji yote na maandalizi yanakamilika kwa wakati ili mradi huo ukamilike kwa muda na uweze kuwanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.
Pia, Mhandisi Seff amewasisitiza wananchi wanufaika wa mradi huo kujitokeza kuunda vikundi kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara kwani watakuwa wanalipwa ili kujiongezea kipato.

Aidha, amewataka wahudhurie mafunzo yatakayokuwa yanatolewa chini ya mradi ili waendelee kulinda barabara ziweze kuwasaidia katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inatekeleza mradi wa RISE unaolenga uboreshaji wa barabara za vijijini kwa ushirikishaji na ufunguaji wa fursa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi “Roads to Inclusion and Social Economic Opportunities (RISE)” katika mikoa minne ambayo ni Mkoa wa Iringa, Geita, Tanga na Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news