Tuendelee kuyaenzi mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa-Waziri Kairuki

NA FRESHA KINASA

WATANZANIA wamehimizwa kuendelea kuenzi mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake na kuwarithisha historia yake vijana na vizazi vijavyo hapa nchini kwa manufaa endelevu.
Hatua hiyo itawezesha kutambua mchango na kazi zake mbalimbali kwa taifa la Tanzania na nchi mbalimbali duniani alioutoa ambao ni urithi wa kudumu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Angela Kairuki kupitia hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mwalimu Mosses Kaegele wakati wa kuhitimisha mashindano ya hiari ya mbio za Mwalimu Nyerere Marathon 2023 zilizofanyika Septemba 30, 2023 Katika Uwanja wa Mwenge uliopo Butiama mkoani Mara.
Ambapo wanariadha kutoka maeneo mbalimbali na viongozi kutoka serikalini na wananchi wamehudhuria na kushiriki mashindano ya mbio hizo.

Kupitia hotuba hiyo, Waziri Kairuki amesema kuwa, mambo mengi mema na ya manufaa yalifanywa na Mwalimu Nyerere kwa taifa lazima yaendelee kurithishwa kwa vijana vizazi vijavyo watambue historia yake na kuzidi kumuenzi katika masuala mbalimbali aliyoyafanya Taifa linajivunia na kuyathamini kwa dhati.
Aidha, Waziri Kairuki amemuagiza Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa, Dkt.Noel Luoga na Mkurugenzi wa Mambo ya Kale, Dkt.Christowaja Ntandu kuwa na mawasiliano na Wilaya ya Butiama katika mbio za marathon zitakazofanyika mwakani ili kuboresha kwa kuwa na matukio mengi muhimu ambayo yatamuenzi Hayati Mwalimu Nyerere.

Dkt. Noel Luoga ambaye ni Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa amesema kuwa, mbio za Mwalimu Nyerere Marathon 2023 zimedhaminiwa na Azania Bank na ni musimu wa pili kufanyika ukiwa na lengo la kutangaza na kurithisha urithi wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Amesema, Mwalimu Nyerere Marathon 2023 imehusisha kilomita 22 mwaka ambao alizaliwa Baba wa Taifa, kilomita 13 tarehe aliyozaliwa Mwalimu Nyerere na kilomita 4 mwezi ambao alizaliwa Baba wa Taifa ambapo barabara iliyotumiwa ni barabara ya Butiama-Busegwe aliyokuwa akiitumia Mwalimu Nyerere kwenda shuleni Mwisenge Mjini Musoma.

Amesema kuwa,Mwalimu Nyerere Marathon 2023 ina lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kuandaa onesho maalum ili kuwafikia watu wenye mahitaji maalum hasa wasioona na wenye uoni hafifu.

Ambapo watapata fursa ya kufundishwa historia ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutambua mambo mbalimbali aliyoyafanya ambayo ni urithi na hazina kwa taifa la Tanzania.

Ameongeza kuwa, Mwalimu Nyerere Marathon 2023 imeshirikisha wakimbiaji zaidi ya 400 pamoja na washiriki zaidi ya 5000 ambapo mwaka jana walikuwa 3000, jambo ambalo linawaleta pamoja wananchi na Watanzania kutambua na kienzi historia yake njema kwa taifa la Tanzania.
Mtoto wa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Madaraka Nyerere akizungumza kwa niaba ya familia amesema, wanafarijika kuona urithi na historia ya Mwalimu Nyerere inaendelea kukua jambo ambalo linamanufaa makubwa kwa Watanzania hasa kizazi ambacho ni kipya kinachopaswa kujifunza kutoka kwake.

Mwenyekiti wa Chama Cha Riadha Mkoa wa Mara, Deograthias Misana amesema kuwa mashindano hayo yatakuwa endelevu katika kuhakikisha vizazi vinarithishwa historia na urithi wake.

Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt.Thereza Israel Mugobi amesema kuwa,Mwalimu Nyerere Marathon ni zao jipya la utalii hivyo lazima liendelezwe kwa ajili ya manufaa ya taifa na kizazi kijacho.
Aidha amesema kuwa, kuna haja kwa kuwa na utaratibu kuyafanya makabila kuwa mazao ya utalii kupitia tamaduni zao mbalimbali ambazo zikitangazwa vyema zitakuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii.

Aidha,zoezi la upandaji wa miti 101 limefanyika, ambapo miti hiyo ni miaka ambayo Baba wa Taifa angekuwa nayo kwa sasa kama angelikuwa hai ifikapo Oktoba 13, mwaka huu na shughuli mbalimbali ikiwemo kuchangia damu salama zimefanyika kiwanjani hapo huku mshindi wa mbio za kilomita 22 akinyakua shilingi milioni moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news