Boeing 737-MAX9 mpya yawasili nchini,Serikali yatoa maelekezo

DAR ES SALAAM-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa maelekezo kwa Wizara ya Uchukuzi, Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi wa ATCL kuhakikisha wanatimiza wajibu wa kusimamia vizuri utoaji huduma za usafiri wa anga ili kuimarisha ushindani Kikanda na Kimataifa na hivyo kuongeza mchango wake katika Pato la Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo Oktoba 3, 2023 wakati wa hafla ya kupokea ndege mpya ya abiria ya masafa ya kati aina ya Boeing 737-MAX9.

Sambamba na uzinduzi wa ndege mbili aina ya Cessna 172S kwa ajili ya mafunzo ya Urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).Hafla hiyo imefanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Terminal 1) Jijini Dar es salaam.

Amewahimiza kufanya kazi kibiashara na kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia sekta hiyo na kuhakikisha wanafikia na kuvuka malengo yaliyowekwa katika Ilani ya ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2020) Ibara ya 58 (a) na (h) (i-ii)) inayotaka kuimarishwa kwa Shirika la ATCL na Sekta ya Usafiri wa anga kwa ujumla.
Makamu wa Rais ameelekeza kumalizwa kwa changamoto wanazokutana nazo abiria wanaotumia shirika la ndege ATCL ikiwemo kuahirisha safari au kusogeza mbele muda wa kuanza safari ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

Ameongeza kwamba, Wizara ya Uchukuzi inapaswa kufuatilia kwa karibu ubora wa huduma zinazotolewa na ATCL na kutoa wito idara ya ununuzi wa vyakula na viburudisho ndani ya ndege za ATCL kuhakikisha inatoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ambazo zimethibitishwa na TBS, ili kukuza kipato na ajira za wajasiriamali au wazalishaji wa Tanzania.
Pia Makamu wa Rais ameelekeza kufanyiwa kazi ndani ya siku kumi na nne changamoto inayotajwa ya gharama kubwa ya usafirishaji wa mizigo kwenda nje ya nchi katika viwanja vya ndege vya JNIA, KIA na Abeid Amani Karume, Zanzibar ikilinganishwa na viwanja vya ndege vya nchi jirani na gharama za kusafirisha mizigo (general cargo) kwa kutumia ndege za mashirika mengine ya Ndege duniani.

Ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha kushirikiana na Wizara husika Zanzibar kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hiyo na kupendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Serikali imetoa fedha za kukiimarisha Chuo cha Usafirishaji cha Taifa (NIT) ili kiweze kutoa mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege, uendeshaji wa safari za ndege pamoja na uhudumu wa ndani ya ndege kwa ithibati za Mamlaka ya Anga nchini ikiwa na lengo la kuzalisha wataalam wengi katika soko la ajira watakaohudumu katika mashirika mbalimbali ya ndege ikiwemo ATCL.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuwekeza kwenye Sekta ya Uchukuzi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutengeneza mazingira mazuri na shindani ya kufanya biashara na uwekezaji nchini.

Amesema, kuwasili kwa ndege hiyo ya kisasa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuendelea kuiwezesha ATCL kutoa huduma bora na ya ushindani huku ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max 9 na Boeing 787-8 Dreamliner zikitarajiwa kuwasili nchini kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2023 na mwezi Machi 2024.
Aidha amesema kwa kutambua fursa zilizopo katika soko la usafiri wa anga na mchango wake katika ukuaji wa uchumi, Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ndogo ya usafiri wa anga ikiwemo ujenzi wa viwanja vya ndege na kuweka mifumo na mitambo ya kisasa ya rada za kuongozea ndege na kulifanya anga la Tanzania kuwa salama.

Halikadhalika, kukamilika kwa ufungaji wa taa za kuongozea ndege katika viwanja vya ndege vya Dodoma na Songwe ni hatua nyingine muhimu itakayowezesha ATCL kuongeza wigo wa safari zake za ndani kwa kuanzisha safari za usiku katika viwanja hivyo.
Ndege mpya ya abiria ya masafa ya kati aina ya Boeing 737-MAX9 ina uwezo wa kubeba abiria 181 ambapo abiria wa daraja la biashara ni 16 na daraja la kawaida ni 165. Ujio wa ndege hiyo unafanya jumla ya ndege zilizonunuliwa na serikali kufikia 14.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news