CCM yafanya teuzi, Jokate Mwengelo ateuliwa kuwa Katibu Mkuu UWT

DAR ES SALAAM-Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliyokutana katika kikao chake maalum, leo tarehe 1 Oktoba, 2023, jijini Dar es Salaam, imefanya uteuzi wa makatibu wakuu wa Jumuiya za Umoja wa Wanawake (UWT) na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Katika kikao hicho, Kamati Kuu kimemteua Ndugu Jokate Mwegelo, kuwa Katibu Mkuu wa UWT, kabla ya uteuzi huo Ndugu Mwegelo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.

Pia, Kamati Kuu imemteua Ndugu Fakii Raphael Lulandala kuwa Katibu Mkuu wa UVCCM, kabla ya uteuzi huo Ndugu Lulandala alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Momba, mkoani Songwe.

Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imemteua Ndugu Hamad Khamis Hamad, kuwa mgombea wa CCM wa nafasi ya Uwakilishi katika Jimbo la Matembwe.

Aidha, Kamati Kuu imewashukuru na kuwapongeza wanachama wote wa CCM na wananchi kwa ujumla katika Jimbo la Mbarali kwa kumchagua mgombea wa CCM Ndugu Bahati Kenneth Ndingo, kuwa Mbunge wao katika uchaguzi mdogo uliofanyika Septemba 20, 2023.

Pia, Kamati Kuu imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na ziara aliyoifanya katika mikoa ya Lindi na Mtwara, ambayo ilikuwa ya mafanikio makubwa sana . Katika ziara hiyo pamoja na mambo mengine, Rais alikagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025, kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi changamoto za wananchi.

Pia, Kamati Kuu kimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa namna anavyoiongoza serikali katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Sophia Edward Mjema
Katibu Wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi

1 Oktoba, 2023

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news