Elimu ya kukabiliana na maafa yawafikia Uvinza

KIGOMA-Wananchi wa Wilaya ya Uvinza wamejengewa uwezo juu ya masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku wakikumbushwa kujiandaa na kukabiliana na athari zinazoweza kutokea kutokana na mvua za El nino zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) zinazotarajiwa kunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi Desemba 2023.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Naibu Kamishna Hamisi Rutengo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa iliyofanyika Ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa katika Jamii Naibu Kamishna Hamisi Rutengo kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu amesema serikali imeendelea kutoa elimu juu ya kujikinga na madhara hayo kwa kuzingatia utabiri uliotolewa hususani kwa mikoa 14 inayotajwa kupata vipindi vya mvua juu ya wastani.
Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Mololo Noah akiwasilisha mada kuhusu Mfumo wa Usimamizi wa maafa nchini wakati wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa iliyofanyika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.

Semina hiyo ilihusisha Wajumbe kutoka katika ngazi ya Kijiji na Kata ambazo ni Uvinza, Kazulamimba na Kandaga upande wa vijini ni pamoja na Mwamila, Mazugwe, Kazuramimba, Nyanganga, Kalenge, Kandaga na Mlela iliyofanyika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Baadhi ya wajumbe wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa kutoka Kata na Vijiji wakifuatilia mada wakati wa semina hiyo.

Naibu Kamishna aliongezea kuwa ni wakati sahihi kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuhama maeneo ya mabondeni, kuendelea kusafisha mitaro ya maji pamoja na kufuatilia taarifa zinazotolewa na mamlaka husiki ili kuendelea kuwa na jamii stahimilivu kwa maafa.
Baadhi ya wajumbe wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa wilaya ya Uvinza wakiwa katika kazi za makundi wakati wa semina ya hiyo.

Aidha aliwakumbusha kuwa jukumu la maafa ni la kila mmoja katika nafasi yake kwa kuzingatia madhara yatokanayo na maafa.

"Kila mmoja anajukumu la kuendelea kukabilia, kujiandaa na maafa hivyo, katika maeneo yetu tuendelee kujilinda na kulinda wengine," alisema Naibu Kamishna huyo.
Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma Bw. Msafiri Nzunuri akieleza namna mkoa ulivyojiandaa kukabiliana na maafa wakati wa semina hiyo.

Kwa Upande wake Mratibu wa Maafa Mkoa wa Kigoma Bw. Msafiri Nzunuri alieleza kuwa mkoa umekuwa ukikabiliwa na maafa mbalimbali ikiwemo Upepo mkali, mafuriko, mioto, pamoja na wanyama wakali ikiwemo Tembo na Viboko kwa maeneo tofauti tofauti na kushukuru elimu iliyotolewa na kusema kuwa itasaidia kuleta hamasa kwa jamii kuwa na utayari katika kukabiliana na maafa.

"Ofisi ya Waziri Mkuu imetupa heshima mkoa wetu kutoongezea maarifa ya namna ya kukabiliana na maafa, itumieni semina hii kwa manufaa na tija katika maeneo yenu, pia msizipuuze taarifa za utabiri wa hali ya hewa nchini," alisema.

Aliongezea kuwa Mkoa umeendelea kuweka mikakatu thabiti ya kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kuyakabili maafa katika nafasi yake endapo yatatokea.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Uvinza Bw. Kenneth Tefurukwa akizungumza jambo na viongozi kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu na ujumbe kutoka shirika la Kimataifa la Uhamaji -IOM (hawapo pichani) walipomtembelea katika ofisi yake kwa lengo la kuendesha semina ya masuala ya menejimenti ya maafa katika Wilaya hiyo.

Naye mratibu wa Maafa Wilaya ya Uvinza Bw. Daniel Yowas akieleleza namna walivyojiandaa katika ngazi ya Wilaya alisema, Zipo kamati za maafa zenye uwezo mkubwa wa kushughulikia masuala hayo huku akizikumbusha kuzingatia elimu iliyotolewa na Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, na kuahidi kuendelea kuyafanyia kazi maelekezo na ushauri wa kitaalam unaotolewa kwa manufaa ya wananchi wote kwa ujumla na kutoa rai kwa kamati hizo kuendelea kutoa taarifa sahihi za tathmin ya majanga na kwa wakati.
Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Bw. Reuben Mbugi akifafanua jambo wakati wa Semina hiyo.
Wajumbe wa Semina ya Kujenga Uelewa juu ya Upunguzaji wa Madhara ya Maafa wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi rasmi wa semina hiyo.(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU).

Awali akitoa neno la utangulizi Mwakilishi kutoka Shirika la Kimataifa la Uhamaji (IOM) Bw. Reuben Mbugi ambalo limefadhili programu hizo ameeleza kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuwafikia wananchi ili kuimarisha utayari wa kukabiliana na maafa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news