Majukumu ya Bodi ya Filamu Tanzania yajadiliwa

DODOMA-Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo imepokea na kujadili majukumu ya Bodi ya Filamu Tanzania na kuipongeza Bodi hiyo kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi za filamu hapa nchini ambayo yamesaidia kuongeza ajira kwa Watanzania.
Akiwasilisha taarifa kuhusu Bodi hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Tasnia hiyo imeitangaza nchi Kimataifa akizitaja filamu za Tanzania zilizofanya vizuri kuwa ni Vuta Nkuvute ya Amil Shivaji ambayo imeshinda Tuzo 14 zikiwemo za nchini Marekani na Ujerumani.

Amezitaja filamu nyingine zilizofanya vizuri Kimataifa kuwa ni Jua Kali iliyofanya vizuri nchini Zambia, Binti Jasiri nchini Nigeria na Nyara nchini Nigeria.

"Bodi imeendelea kulea wasanii na kusimamia haki zao ambapo katika malalamiko 83 yaliyopokelewa na Bodi 81 yamefanyiwa kazi, ambapo wale wanaofanya vizuri tumekua tukiwatuza kupitia Tuzo za filamu za kila mwaka ambazo tayari zimefanyika kwa mara mbili na mwaka huu zitafayika mwezi Novemba" amesema Mhe. Mwinjuma

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Husna Sekiboko ameitaka Wizara iendelee kusimamia vyema utengenezaji wa Filamu Bora, zinazoitangaza Tanzania na mandhari yake pamoja na kulinda maadili ya nchi.

Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati hiyo wakichangia taarifa hiyokwa nyakati tofauti wameshauri Serikali iendelee kuwatambua na kuwapa nafasi wasanii chipukizi katika majukwaa ya Kimataifa pamoja na kuongeza upatikanaji wa mafunzo kwa Wadau wao ili wafanye vizuri na kuhimili ushindani katika soko la Kimataifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news