MPC:Akiba ya fedha za kigeni imezidi kuimarika nchini

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu imebaini kuwa, uhaba wa fedha za kigeni ulioonekana hivi karibuni nchini umeendelea kupungua kufuatia ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii,mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba baada ya kamati kufanya mkutano wake wa 228 tarehe 27 Oktoba 2023.

Lengo la mkutano huo ulikuwa ni kutathmini utekelezaji wa Sera ya Fedha na mwenendo na mwelekeo wa uchumi. 
 
Pia amebainisha kuwa, akiba ya fedha za kigeni imeendelea kubaki katika viwango vya kuridhisha vya takribani dola za Marekani bilioni 5 katika kipindi cha mwezi Julai mpaka Oktoba 2023, kiwango kinachotosha kugharamia uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi, juu ya viwango vya nchi na jumuiya ya Afrika Mashariki vya miezi 4 na 4.5 mtawalia.
 
Aidha, Sekta ya benki iliendelea kuwa na mtaji, ukwasi wa kutosha na inayotengeneza faida. 
 
Ubora wa rasilimali umeendelea kuimarika, kufuatia kupungua kwa viwango vya mikopo chechefu kufikia asilimia 5.2 mwezi Septemba 2023,kutoka asilimia 7.3 mwezi Septemba 2022.

Kamati ilibaini kuwa, utekelezaji wa sera ya fedha ulichangia kuwepo kwa kiasi cha kutosha cha ukwasi kwenye uchumi kwa mwezi Agosti, Septemba na Oktoba 2023.

"Uuzaji wa fedha za kigeni uliofanywa na Benki Kuu kwa lengo la kukabiliana na ongezeko la mikopo inayotokana
na uagizaji wa bidhaa nje ya nchi pia umepunguza changamoto hii,"amebainisha Gavana Tutuba.

Aidha, amefafanua kuwa, hali ya upatikanaji wa fedha za kigeni inatarajiwa kuendelea kuimarika kutokana na matarajio ya mapato yanayotokana na shughuli za utalii, uuzaji wa madini na mazao ya biashara.

Sambamba na hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu na Serikali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni.

"Kwa kuzingatia mwenendo wa uchumi wa dunia na wa hapa nchini, Kamati ya Sera ya Fedha iliamua kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kasi ya ongezeko la ukwasi katika uchumi,"ameongeza. 

Wakati huo huo, MPC imebainisha kuwa, utekelezaji wa sera ya fedha, pamoja na sera thabiti za kibajeti, na kimfumo, zimesaidia kukabiliana na shinikizo la mfumuko wa bei, kuchangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na uhimilivu wa sekta ya fedha nchini licha ya mtikisiko wa kiuchumi duniani.

Aidha, utekelezaji wa sera ya fedha pia umesaidia kupunguza shinikizo linalotokana na ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni nchini.

Kamati pia, ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia kwa mwaka 2023 na kubaini kuwa, uchumi wa dunia bado haujaimarika licha ya ukuaji wa juu ya matarajio uliofikiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka. 

Mwenendo huu unatokana na kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani, migogoro ya kisiasa na ongezeko la bei za mafuta.

Pia, amebainisha kuwa, Sera ya fedha itaendelea kutekelezwa sambamba na sera za kibajeti na kimuundo ili kufikia malengo ya kiuchumi.

Aidha,amesema utekelezaji wa Sera ya Fedha unalenga kuhakikisha malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya Extended Credit Facility (ECF) kwa robo inayoishia Desemba 2023 yanafikiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news