Musoma Vijijini watolewa hofu ujenzi barabara ya lami hadi Busekera

NA FRESHA KINASA

WAZIRI wa Ujenzi, Mheshimiwa Innocent Bashungwa amewatoa wasiwasi wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini kuhusu ujenzi wa barabara kuu ya Musoma-Makojo Busekera yenye urefu wa kilomita 92 kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Bashungwa amesema, serikali itaendelea kujenga barabara hiyo kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi jimboni humo na Mkoa wa Mara kiujumla.

Ameyasema hayo Oktoba 10,2023 alipofanya ziara ya kikazi Musoma Vijijini kwa lengo la kuwatoa wasiwasi wananchi kuhusu ujenzi wa barabara yao kuu kwa kiwango cha lami ambayo imekuwa ikitumika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Barabara ya Musoma-Makojo-Busekera yenye urefu wa kilomita 92 ndiyo barabara kuu inayounganisha vijiji 68 vya Jimbo la Musoma Vijijini na Miji ya Musoma na Mwanza.

Aidha, Waziri Bashungwa amempongeza Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kwa namna anavyofuatilia ujenzi wa barabara hiyo na miradi mbalimbali ya Maendeleo inayotekelezwa na Serikali kwa ajili ya kuwanufaisha Wananchi.

"Niwaondoe wasiwasi wananchi juu ya ujenzi wa barabara hii, kwa wale wa maeneo ya Bukima lami itakapopita patawekwa taa kina mama na vijana wanaojishugulisha mchana hata usiku mkitaka mtaweza kujishughukisha, usiku panakuwa kama mchana ili kufanya kazi ya kujiingizia kipato,"amesema Waziri Bashungwa.

Nao Wananchi wa Musoma Vijijini wameishukuru Serikali kwa dhamira njema ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwani itasaidia usafirishaji wa mazao yao na kukuza shughuli za kiuchumi pamoja na kuchochea Kasi ya maendeleo.

"Musoma Vijijini tunavua dagaa, na dagaa hawa wanasafirishwa kwenda mikoa mingine, pia Kuna shughuli za kilimo zinafanyika wakati wa mvua barabara inakuwa na shida kupitisha mazao yetu. Kwa hiyo kukamilika kwa barabara hii kutaleta manufaa kwetu Wananchi. niiombe serikali ujenzi wake ufanyike haraka kwani umekuwa wa taratibu sana," amesema Emmanuel Jackson Mkazi Makojo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Oktoba 11, 2023 imeeleza kuwa

"Ujenzi wa barabara hilo kwa kiwango cha lami unasuasua sana kwani ni kilomita tano (5) tu zilizokwishajengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa kilomita hizo tano (5) ulichukua miaka minne (4)," imeeleza taarifa hiyo na kusema kuwa.

"Barabara hili ndilo roho kuu ya uchumi na ustawi wa wananchi wa Musoma Vijijini, na liko kwenye Bajeti ya Mwaka huu (2023/2024),"imeeleza taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news