Papa Mtakatifu Francis awasimika makardinali wapya 21

VATICAN-Septemba 30,2023 Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Mtakatifu Francis amewasimika makardinali wapya 21 ambao aliwateua Julai 9, 2023.

Kati yao Makardinali watatu ni wale ambao wamejipambanua katika huduma kwa kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wao.

Makardinali wapya wamesimikwa rasmi katika mkutano wa kawaida wa Makardinali uliofanyika mjini Vatican.

Papa Mtakatifu katika mahubiri yake amekazia zaidi uwakilishi wa Makardinali toka sehemu mbalimbali za dunia, kama ilivyokuwa siku ile ya Pentekoste ya kwanza.

Amesema, hawa ni Makardinali na Maaskofu wa nyakati hizi, ili kugundua kwa mshangao zawadi ya Injili waliyoipokea katika lugha zao wenyewe, tayari kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Wakiwa tayari kusimama kidete na kuwa ni wainjilishaji, huku wakimwilisha ndani mwao, ujenzi wa Kanisa la Kisinodi pamoja na kuendelea kumwaminia Roho Mtakatifu anayetengeneza uotofauti na umoja; kiongozi mpole na thabiti.

Kardinali Robert Francois Prevost, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu kwa niaba ya Makardinali wapya amemshukuru Papa Mtakatifu kwa kuwateuwa kuwa ni wahudumu wa kanisa katika kutangaza na kushuhudia kwa furaha habari njema ya wokovu.

Sambamba na kuwashirikisha katika dhamana ya kuliongoza kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa kujikita zaidi katika fadhila ya unyenyekevu.

Kikao hiki cha Makardinali kinafanyika mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.”

Jambo la msingi ni kujenga utamaduni wa kusikilizana kama njia ya kuiishi imani sanjari na ukuaji wa kidugu kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wagonjwa na mazingira.

Miongoni mwa waliosimikwa ni pamoja na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi kwake.

"Natoa za dhati kwa Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, kwa kusimikwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Kardinali.

"Kauli mbiu ya utume wako ni "Enendeni ulimwenguni kote", ikiakisi mafundisho ya Yesu Kristo katika Injili ya Marko 16:15, juu ya utume unaojali watu wote, sehemu zote na wakati wote.

"Naungana na Watanzania wote kukuombea kheri, afya njema, na mafanikio katika utumishi wako."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news