Rais Frank-Walter Steinmeier kuwasili Tanzania kesho kwa ziara ya kikazi

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini kuanzia Oktoba 30 hadi Novemba 1,2023.

Picha na CZAREK SOKOLOWSKI / AP.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Mambao ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imefafanua kuwa, ziara hii mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa kimaendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani,pia imelenga kwenye kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.

Ujumbe wa Mheshimiwa Rais Steinmeier utakao jumuisha viongozi wengine wa Serikali, pamoja na wawekezaji wa makampuni makubwa 12 utawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Oktoba 2023 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba (Mb.).

Akiwa nchini, Mheshimiwa Rais Steinmeier atafanya mazungumzo rasmi na Mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 31 Oktoba 2023. 

Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watapata fursa ya kuongea na waandishi wa habari kuelezea kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao.

Kadhalika, Waheshimiwa Marais watapata fursa ya kushiriki katika Jukwaa la Biashara, litakalohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika Hoteli ya Hyatt Regency; ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi hao watapokea taarifa iliyojadiliwa na Jukwaa hilo.

Siku hiyo hiyo, Mheshimiwa Rais Steinmeier anatarajiwa kuonana na kuzungumza na vijana wajasiriamali wa Kitanzania wanaojihusisha na uvumbuzi wa teknolojia mpya hususan matumizi ya akili bandia ambao wanafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani.

Vilevile, Mheshimiwa Rais Steinmeier atatembelea Kiwanda cha Twiga Cement Jijini Dar es Salaam kinachoendeshwa kwa ubia na Kampuni ya Scancem International ya Ujerumani.

Novemba 1, 2023, Mheshimiwa Rais Stenmeier atasafiri kwenda Wilayani Songea Mkoani Ruvuma kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji na Shule ya Msingi ya Majimaji.

Hii ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ujerumani zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliodumu kwa muda wa miaka zaidi ya 60.

Nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana kwenye sekta mbalimbali za kimkakati hususan biashara na uwekezaji, maji, afya, usawa wa kijinsia, uwezeshaji wanawake, uhifadhi wa bioanuai, usimamizi wa fedha, utalii pamoja na malikale na utamaduni.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka.

Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni pamoja na Kahawa, Tumbaku, Pamba, Asali, Samaki, Nta na vito vya thamani.

Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu zinazoagizwa kutoka Ujerumani ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi) Magari, Vifaa na Mashine za Umeme.

Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini. Kwa mujibu wa TIC hadi kufikia Agosti 2023, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 408.11 ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira zipatazo 16,121.

Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imefanikiwa kusajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 300.00 ambayo imezalisha ajira 905.

Kampuni za Kijerumani zilizowekeza nchini zinajihusisha zaidi na sekta za kilimo, viwanda, nishati mbadala, ujenzi, utalii sanaa na utamaduni.

Kufanyika kwa ziara hii ni ushahidi tosha kuwa Diplomasia ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inazidi kupaa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news