Waziri Prof.Mkumbo ashuhudia uwekaji saini mkataba wa Bilioni 95/- Mradi wa Umeme wa Kakono

BRUSSELS-Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo (Mb) ameshuhudia uwekaji saini wa mkataba baina ya EU na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambapo EU imetoa msaada (grant) kwa Tanzania wa Euro milioni 36 sawa na Shilingi bilioni 95 kwa ajili ya Mradi wa Uzalishaji wa Umeme kwa njia ya Maji wa Kakono, mkoani Kagera wa MW 87.8).

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo (kushoto) akifurahia baada ya uwekaji saini wa mkataba baina ya EU na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ambapo EU imetoa msaada (grant) kwa Tanzania wa Euro milioni 36 sawa na Shilingi bilioni 95 kwa ajili ya Mradi wa Uzalishaji wa Umeme kwa njia ya Maji wa Kakono, mkoani Kagera wa MW 87.8).

Uwekaji saini huo ulifanyika wakati wa Mkutano wa Global Gateway Forum uliofanyika Brussels, Ubelgiji tarehe 25 na 26 Oktoba 2023 ambapo Prof. Mkumbo alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano huo.

Mradi huo wenye gharama ya jumla ya Euro million 288.11 sawa na takribani shilingi bilioni 800 unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia mikopo nafuu kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na msaada wa EU.

Mheshimiwa Mkumbo ameishukuru EU kwa msaada wake kwenye Mradi huo na kuahidi kuwa Serikali itasimamia kikamilifu utekelezaji wake.

Aidha, Mhe. Waziri alishiriki na kuchangia kwenye mijadala yenye lengo la kuweka mikakati ya pamoja kwenye masuala ya madini ya kimkakati na mageuzi ya kidijitali. Kuhusu madini ya kimkakati, majadiliano na makubaliano yamefikiwa kwamba Mpango wa Global Gateway uchochee uwekezaji unaowezesha madini ya kimkakati kuongezewa thamani katika nchi yanakochimbwa badala ya thamani kuongezwa baada ya madini hayo kuuzwa nje.

Tanzania ni nchi yenye karibu aina zote za madini hayo ikiwemo lithium, graphite, cobalt na nickel, Mhe. Waziri ameuhakikishia Mkutano huo utayari wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupokea uwekezaji huo na tayari mazingira mazuri na rafiki ya uwekezaji yamewekwa.

Kwa upande wa mageuzi ya kidijitali, Mhe. Waziri ametumia Jukwaa hilo kuishukuru EU kwa msaada wa Euro milioni 35 sawa na shilingi bilioni 80 ilizotenga kuisaidia Tanzania kwa ajili ya kuchochea mageuzi ya kidijitali. Wajumbe waliafikiana kuwa mageuzi ya kidijitali yatumike kuongeza kasi ya uwekezaji katika maeneo yanayochochea maendeleo ya kidijitali kama vile kilimo, elimu, biashara, afya na mengineyo na kuhimiza mageuzi ya kidijitali yachochee zaidi maendeleo ya wananchi wakiwemo wa vijijini.

Mhe Waziri alitumia fursa hiyo pia kufanya mikutano ya pembezoni na uongozi wa juu wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) na kueleza mipango na vipaumbele mbalimbali vya kitaifa na kuomba Benki hiyo iendelee kushirikiana na Serikali yetu katika utekelezaji wa mipango na vipaumbele hivyo kupitia mikopo ya masharti nafuu.

EIB ni mmoja wa wabia wa maendeleo na kupitia mikopo nafuu ya Benki hiyo miradi mbalimbali hivi sasa inatekelezwa ikiwamo ya ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege, miradi ya maji na mikopo kwa ajili ya wajasiriamali kupitia benki za Tanzania.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila A. Mkumbo (wa pili kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas A. Nyamanga (wa kwanza kulia) wakifutilia majadiliano ya Mkutano wa Global Gateway Forum uliofanyika Brussels, Ubelgiji tarehe 25 na 26 Oktoba 2023.

Vile vile, alizungumza na Mkurugenzi anayeshughulikia Ubia wa Kimataifa ndani ya EU kwa nchi za Afrika na kujadiliana mipango na vipaumbele vya Tanzania. Wakati wa majadiliano hayo, Prof. Mkubo aliishukuru EU kwa msaada (grant) wa kiasi cha Euro milioni 703 ambazo ni takribani shilingi trilioni 1.9 ilizopanga kusaidia kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania kwa kipindi cha mwaka 2021 hadi 2027.

Global Gateway Investment Package ni mpango wa EU wa kuchochea uwekezaji duniani hususan barani Afrika ambako Mpango huo unalenga kuchochea uwekezaji wa jumla ya Euro billioni 150 barani Afrika. Nchi zaidi ya 90 zilihudhuria mkutano huo kwa ngazi ya Marais, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri pamoja na viongozi wengine kutoka Mashirika ya Kimataifa na sekta binafsi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news