Spika Dkt.Tulia ashinda urais Umoja wa Mabunge Duniani (IPU)

NA GODFREY NNKO

SPIKA wa Bunge la Tanzania Dkt.Tulia Ackson ameshinda kwa kishindo kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), uchaguzi uliofanyika Oktoba 27,2023 jijini Luanda nchini Angola.

Mhe. Dkt Tulia ameshinda uchaguzi huo mara baada ya kupata kura 172 ambazo ni sawa na asilimia 57 ya kura 303 zilizopigwa na wajumbe walioshiriki Mkutano wa 147 wa IPU.

Dkt. Tulia amewashinda wagombea wengine watatu waliogombea nafasi hiyo ambao ni Mhe. Adji Diarra kutoka Bunge la Senegal aliyepata kura 59, Mhe. Catherine Hara Spika wa Bunge la Malawi aliyepata kura 61 na Mhe. Marwa Hagi kutoka Bunge la Somalia aliyepata kura 11.

Mhe. Dkt. Tulia anakuwa Rais wa 31 wa IPU na pia Mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika kushika wadhifa huo.

Aidha, Mheshimiwa Spika Dkt.Tulia aliwasili jijini humo Oktoba 19, 2023 amewasili kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 147 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) ambao ulianza Oktoba 20, 2023 na unatarajiwa kufikia tamati Oktoba 29, 2023.

Mkutano huo una dhima kuu kuhusu “Hatua za Kibunge kuchagiza Amani, Haki na kujenga Taasisi Imara” (Lengo la 16 la Maendeleo Endelevu).

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amempongeza Dkt.Tulia kwa ushindi huo.

"Pongezi za dhati kwa Spika wa Bunge letu, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

"Ushindi huu ni ushuhuda wa kazi kubwa unayoendelea kuifanya na imani wajumbe waliyo nayo juu yako na nchi yetu.

"Kuchaguliwa kwako pia ni matokeo ya miaka mingi ya kazi, weledi na kujituma katika utumishi wa umma, mfano bora kwa watoto wa kike katika nchi yetu, Afrika na hata nje ya mipaka ya bara letu,"ameleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news