TAKUKURU yawauma sikio wanafunzi mkoani Mara

NA FRESHA KINASA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mara imewataka wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne katika shule za Sekondari Mkoani humo kwenda kuwa chachu ya kuongeza mapambano ya vitendo vya rushwa katika maeneo yao,jamii na taifa kwa ujumla.
TAKUKURU pia imesema, kumekuwepo na baadhi ya vitendo vya rushwa maeneo mbalimbali ikiwemo rushwa ya ngono katika vyuo vya kati na vyuo vikuu, lakini kupitia elimu ya kupambana na rushwa waliyoipata katika shule zao kupitia Klabu za Wapinga rushwa iwasaidie kukabiliana na tatizo hilo kwa maendeleo ya nchi na Ustawi bora.

Hayo yamesemwa Oktoba 7, 2023 na Mwanyika Senzota, Àfisa Mchunguzi kutoka Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Mara kwa niaba ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa huo katika mahafali ya kuwaaga wahitimu ambao ni wanachama wa Klabu za Wapinga rushwa kutoka shule tatu za Sekondari zilizopo Manispaa ya Musoma.
Shule hizo ni pamoja na Shule ya Sekondari Iringo, Mwisenge na Mshikamano ambapo mahafali hayo yamefanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa wa Mara uliopo Mjini Musoma.

Ameongeza kuwa, jukumu la kupambana na vitendo Vya rushwa linapaswa kufanywa na kila mmoja katika sehemu yake alipo iwe kazini, badala ya kuiachia TAKUKURU pekee jukumu hilo na hivyo nguvu zaidi ya utoaji wa elimu maeneo mbalimbali inapaswa kuendelea kutolewa ili kuhakikisha rushwa inatokomezwa.
Aidha, amewataka Walimu wa shule za Msingi na Sekondari Mkoani humo kuendelea kuzilea kikamilifu Klabu za wanafunzi Wapinga rushwa kwani zinawaandaa vyema vijana kuja kuwa wazalendo na waadilifu katika kulitumikia Taifa katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

"Mmejifunza mambo mengi kuhusiana na rushwa, madhara yake katika Jamii lakini pia ushiriki wenu katika kupambana. Niwaombe mkawe mabalozi wema mnakokwenda wapo mtaendelea na masomo ya kidato Cha tano hadi vyuo vikuu kasaidieni pia kukabiliana na rushwa ya ngono ambayo pia ni kosa kisheria. Kaweni waadilifu na wazalendo kupambana na rushwa,"amesema.
Kwa upande wake Amos Ndege ambaye ni Àfisa Idara ya Elimu kwa umma kutoka TAKUKURU Mkoa wa Mara amesema, lengo la kuanzishwa Klabu za Wapinga rushwa Mashuleni ni kuwafanya wafahamu wajibu katika kuzuia na kupambana na rushwa kwani jukumu hilo ni la kila mmoja.

Pia, Ndege amewataka wanafunzi ambao wako vidato vya chini wajiunge na Klabu ya Wapinga rushwa katika shule zao waweze kujifunza mambo mengi ambayo yatawasaidia waweze kupambana Kama ambavyo serikali imekuwa ikisisitiza mapambano ya rushwa kwa ajili ya kuwa na ufanisi katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
Mwalimu Makuru Lameck Joseph ni Mratibu wa Klabu za Wapinga Rushwa Manispaa ya Musoma na Mwalimu Mlezi wa Klabu ya Wapinga rushwa katika shule ya Sekondari Iringo iliyopo katika Manispaa hiyo, ameishukuru TAKUKURU Mkoa wa Mara kwani imeendelea kuwa pamoja na shule za Manispaa ya Musoma ikiwemo kuzitembea Klabu za Wapinga rushwa na kutoa elimu na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi wajiunge na Klabu hizo.

Dorcas Edwin akisoma risala ya wahitimu ambao ni wanachama wa Klabu ya Wapinga rushwa kutoka shule ya Sekondari Mwisenge amesema kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuwa mabalozi wema wa mapambano dhidi ya rushwa katika maisha yao sambamba na kutoa hamasa kwa jamii kuchukia rushwa kwa faida ya Jamii na taifa pia.
Pia, ameishukuru TAKUKURU Mkoa wa Mara kwa kuendelea kuwathamini wahitimu ikiwemo kuwapa vyeti ambavyo ni chachu katika kuwapa hasa ya kupambana na rushwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news