Waziri Dkt.Jafo ateta na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered

DAR ES SALAAM-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende na kujadili fursa za uwekezaji na uwezeshaji wa miradi ya mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi hapa nchini.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisikiliza jambo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered Bw. Herman Kasekende wakati wa kikao baina yake na watendaji wa Benki hiyo kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais, Jijini Dar es Salaam leo Jumanne (Oktoba 10, 2023).

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika leo Jumanne (Oktoba 10, 2023), katika ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, Waziri Jafo aliipongeza juhudi za benki hiyo katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi hapa nchini.

Dkt. Jafo amesema mapambano ya uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi yanahitaji juhudi za pamoja baina ya serikali na wadau na kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendeleza ushirikiano na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi za kifedha ili kuibua fursa za uwezeshaji na uwekezaji wa miradi ya mazingira nchini.Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw.Herman Kasekende (kushoto) akizungumza jambo wakati wa kikao baina yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo kilichofanyika katika katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais, Jijini Dar es Salaam leo Jumanne (Oktoba 10, 2023). Kulia ni Meneja Mipango ya Biashara wa Benki hiyo, Bw. Michael Matteru.

Akitolea mfano, Waziri Jafo amesema Serikali imeandaa kanuni na mwongozo kuhusu biashara ya kaboni ikiwa ni mkakati wa kuboresha usimamizi mzuri wa miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa nchini, na kuzitaka taasisi za kifedha kujitokeza katika kuziwezesha mitaji kwa kampuni mbalimbali ya Watanzania.

“Utekelezaji wa biashara ya kaboni utachangia kupunguza gesijoto na hatimaye kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na pia kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu. Jukumu hili linahitaji mshikamano wa wadau wote,”amesema Dkt. Jafo.

Aidha, Dkt. Jafo ameiomba benki hiyo kuweka mpango na mikakati madhubuti ya uwekezaji katika nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira kwani nishati isiyo salama kwa matumizi ikiwemo kuni na mkaa imekuwa na madhara kwa afya kwa watumiaaji na kuharibu mazingira.

“Serikali imendaa rasimu ya Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia 2030.Tunaendelea kuwahimiza wadau ikiwemo taasisi za kifedha kujitokeza na kuwekeza katika miradi ya uzalishaji wa bidhaa na nishati safi ya kupikia na hivyo kurahisisha upatikanaji wake kwa Watanzania” amesema Dkt Jafo.Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani
Jafo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji waandamizi wa Benki ya Standard Chartered wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Bw. Herman Kasekende (kulia) muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao baina yao kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais, Jijini Dar es Salaam leo Jumanne (Oktoba 10, 2023).(Picha na OMR).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende amemhakikishia Waziri Jafo kuwa Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhamasisha utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akitolea mfano Kasekende amesema Benki ya Standard Chartered tayari imeandaa andiko la miradi ya uwekezaji wa mazingira na mabadiliko ya nchi ikiwa ni hatua mahsusi ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwashirikisha wadau kuibua miradi uhifadhi wa mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia jamii ya Watanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia uwekezaji wa miradi…Tutatoa mitaji kwa makampuni ya Watanzania yatakayoanzisha miradi ya biashara ya kaboni,”amesema Kasekende.

Aidha, Kasekende amesema Benki hiyo pia imeanzisha kampeni maalum ya upandaji miti ambapo katika msimu wa mvua uliopita taasisi hiyo imepanda miti 2,000 na msimu ujao wa mvua imepanga kupanda miti 10,000 katika maeneo mbalimbali nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news