Waziri Mbarawa:Ujenzi wa SGR kipande cha Makutupora-Tabora unaendelea vizuri

SINGIDA-Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema kuwa, Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kipande cha tatu Makutopora mkoani Singida mpaka Tabora kilomita 368 unaendelea vizuri japo kuna changamoto mbalimbali.
Waziri Mbarawa ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo ambapo amesisitiza kuwa licha ya changamoto zilizobainika bado serikali itahakikisha changamoto hizo zinatatuliwa na mradi unakamilika kwa wakati.

"Kasi ya ujenzi tuliyoitarajia imepungua,leo hii tulitakiwa kufikia asilimia ishirini na mbili lakini leo tumefikia asilimia kumi na mbili kuna asilimia kumi zimepungua.

"Hii ni changamoto lakini tukiweka mikakati vizuri tunaweza kulitatua," amesema Prof. Mbarawa.

Aidha Mbarawa amesema kuwa hakuna taarifa yoyote kwamba mkandarasi ameshindwa kuendelea na mradi kwani kazi bado inaendelea huku akionyesha ushahidi wa kazi zinavyoendelea katika kituo cha Tabora ambapo ujenzi wa tuta unaendelea.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) , Mhandisi Senzige Kisenge amesema. kutokana na changamoto iliyobainika TRC imemuelekeza mkandarasi kuandika mpango wa namna atakavyofidia muda uliopotea kama sehemu ya kutatua changamoto hiyo ili mradi ukamilike kwa wakati.

Mhandisi Kisenge amesema kama waziri alivyoelekeza kufanyika kikao na mkandarasi huyo huku kikao kikiongozwa na waziri ili kuhakikisha kila kitu kinawekwa sawasawa na kazi inafanikiwa.

Meneja Mradi wa ujenzi wa SGR kipande cha Makutupora-Tabora, Mhandisi Edwin Ntahondi amesema hatua inayoendelea kwa sasa ni ujenzi wa tuta kuu ambapo katika kilomita 368 za mradi mkandarasi amegawanya ujenzi huo katika maeneo matano na yote yana watu wanaoendelea na kazi hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news