2,400 kulipwa fidia kupisha uendelezaji Bonde la Mto Msimbazi

NA GODREY NNKO

ZAIDI ya wananchi 2,400 ambao wanapisha Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi jijini Dar es Salaam wanatarajia kuanza kulipwa fidia zao kesho Novemba 16,2023.

Hayo yamesemwa leo Novemba 15, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza na wakazi hao katika eneo la Jangwani jijini humo.

Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amesema,fidia hiyo inalipwa kwa wananchi wote waliokubali kulipwa na kufanyiwa uhakiki wa taarifa zao za kibenki ili kupisha utekelezaji wa mradi huo na tayari Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kwa ajili hiyo.

"Msingi wa Serikali yoyote duniani ni msingi wa ustawi wa watu wao, kwa hiyo tuko hapa kutekeleza maelekezo yanayotuelekeza kutoka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

"Lakini, tuko hapa kutekeleza misingi ya kanuni za TANU ambazo zimezungumza sana kuhusu ustawi wa maisha ya wananchi wetu na wananchi wamezungumzwa sana katika kila sehemu.

"Ukisoma, vitabu vyetu ukisoma Ilani ya Uchaguzi ukisoma Katiba ya nchi imezungumzwa sana kuhusu wananchi na ustawi wa maisha yao.

"Sasa, fikira hizi za Rais wetu Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ni mwendelezo wa utekelezaji wa fikira za Baba wa Taifa (Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) ambaye yeye misingi yote hii tunayoiona, ustawi wa maisha iliyoingizwa kwenye Katiba ya mwaka 1977, lakini Kanuni za TANU na mambo mengine mengi.

"Haya yanayoendelezwa leo ni kwa sababu misingi aliyotuachia Baba wa Taifa inaendelezwa na viongozi wetu walioko sasa, Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Kwa hiyo leo amenituma nije hapa,kwanza niwashukuru waheshimiwa wabunge na waheshimiwa madiwani. Ninawashukuru wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu eneo hili wamelipigia kelele sana wanataka kujua ni lini wananchi wanalipwa.

"Kwa hiyo tuwashukuru sana waheshimiwa wabunge, wanafanya kazi nzuri sana ya uwakilishi. Nimpongeze na kumshukuru sana Naibu Spika, Mheshimwa Mbunge wa Jimbo la Ilala, Mheshimiwa Zungu anafanya kazi kubwa na kazi nzuri sana.

"Lakini, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge wa Kinondoni, Mheshimiwa Tarimba mara zote amekuwa akigonga mlango ofisini kwangu kuuliza ni lini wananchi wangu wanalipwa.

"Lakini, nimshukuru sana Mheshimiwa Bonnah, Mhehimiwa Bonnah, Mbunge wa Jimbo la Segerea yeye juzi wakati anachangia kwenye mpango wa maendeleo alinifuata kwenye kiti akaniuliza ni lini wananchi wetu wanalipwa, kwa sababu wananchi wanaoishi hapa Jangwani wengine wana familia zao kwenye majimbo mbalimbali.

"Kwa hiyo, tunawashukuru sana viongozi hawa wawakilishi, Katibu wa Mkoa (CCM) ninataka nikuthibitishie wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam wanafanya kazi kubwa kwa maslahi ya wananchi wetu."

Katibu CCM

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam,Adam Ngalawa amesema kuwa, "Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, tumekuja hapa na Mheshimiwa Waziri nia ni kwamba tunapata majawabu yanayoweza kuwafanya muendelee kuishi kwa amani na utulivu.

"La pili tunafahamu kwamba, eneo hili kwa muda mrefu si eneo rafiki sana,tuzingatie maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ili tuweze kuishi kwa amani na usalama zaidi.

"Na, la tatu Mheshimiwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ana nia njema kwa Watanzania na kwa lolote analolifanya kupitia kwa mawaziri wake ni kutaka maisha bora kwa kila Mtanzania, kwa hiyo leo muishi na mtegemee maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri,"amebainisha Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam.

Waziri Mchengerwa tena


"Lakini, pili lililonileta hapa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, utekelezaji wa Ibara ya 8 ya Katiba na ibara nyingine za Katiba zinazozungumzia kuhusu wananchi...wananchi.

"Na sisi TAMISEMI tulikwishasema, kwamba wizara hii TAMISEMI ni wizara ya wananchi, kwa sababu ndiyo inagusa maisha halisi ya Watanzania wa kawaida kabisa katika maeneo mbalimbali,"amefafanua Waziri Mchengerwa.

Mhandisi Kanyenye

Akizungumzia kuhusu utaratibu uliopo kwenye huo Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, Mratibu anayesimamia miradi inayotekelezwa na Benki ya Dunia, Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema wananchi wa mitaa 16 watalipwa malipo mbalimbali kutokana na thamani ya vitu walivyonavyo.

Kuhusu posho ya kujikimu kwa wakazi hao ambao wanapaswa kupisha mradi huo, Mhandisi kanyenye amesema, "Hii posho haijapatikana si flat kwa watu wote ni thamani ya nyumba yako na market rate, kwa mfano kama nyumba yako unalipwa kodi ya laki moja.

"Maana yake utalipwa laki moja mara miezi 36, hauwezi kulipwa sawa na kila mtu ndivyo ilivyofanyika mimi siyo mthamini, lakini ndivyo ninaelewa inavyofanyika.

"Kwa hiyo hiyo thamani ya accomodation iliyolipwa ndiyo sahihi kwa mujibu wa sheria na ndiyo mthamini mkuu wa Serikali ameidhinisha.

"Hilo ni la kwanza, lakini la pili Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amezungumzia kuhusu posho ya ardhi, Mheshimiwa Waziri sisi tuko tayari kupokea maelekezo yako kuhusu suala la ardhi, ni kweli kwamba eneo hili nyumba zote zilizolipwa hazijalipwa na thamani ya ardhi.

"Zimelipwa kama ni nyumba, ni nyumba tu peke yake, kwa hiyo suala la ardhi tunaomba Mheshimiwa Waziri ukishatoa maelekezo na nini cha kufanya na sisi watumishi wako tuko tayari kutekeleza utakachotaka kutuelekeza.

"Kulikuwa na suala la watu wa Mabwepande ninafikiri, wale watu wa Mabwepande tumesitisha malipo yao kwa sasa kwa sababu ya taratibu ambazo tunataka kuzifuata kama ni kuwalipa, lakini kuna taratibu za kuzifuata.

"Kwa sababu wale walishawahi kupewa ardhi, Mheshimiwa Waziri walipewa ardhi maeneo ya Mabwepande, lakini wengi wao walirudi na taarifa zao zimekuwa zikichanganyachanganya, kwa hiyo tunahitaji kutumia muda wa kutosha kupitia taarifa zao na kujiridhisha.

"Kuhusu kila mmoja nini alipata, na kama kuna kitu anastahili sasa hivi kukipata na chenyewe tuangalie ni kiasi gani, kwa hiyo wale tu ambao hawakuhamishiwa Mabwepande ndiyo ambao zoezi hili la malipo litawahusu,"amefafanua Mhandisi Kanyenye.

RC Chalamila


Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amewaeleza wananchi hao kuwa, ardhi haijajumuishwa katika kulipa fidia kwa sababu wataalamu wanasema maeneo hayo ni oevu.

Pia, Chalamila amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa anaoufanya katika mkoa huo wenye masilahi mapana ya umma ambapo amewataka wananchi na wakazi wa Bonde la Mto Msimbazi kutii kauli ya Serikali.

"Hauwezi kuyalipia fidia, kwa sababu ni maeneo ambayo ni kama kumtuma Afisa Ardhi akapime halafu atoe hati, maeneo hayo hayawezi kupimwa na kutolewa hati kwa utaratibu uliopo sasa.

"Na kwa mujibu wa Chief Valuer wa Serikali maeneo haya ni oevu ambayo thamani yake inakuwa haiingi kwenye fomula ya kulipa malipo ya fidia.

"Na ndiyo maana kwa mujibu wa mtaalamu huyu anasema, Mheshimiwa Waziri sisi tumefuata utaalamu wote na ndiyo maana mpaka mwisho hakuna category ya kulipwa fidia ya ardhi."

Vile vile, RC Chalamila amewataka wananchi hao kutokukubali kurubuniwa au kudanganyana, kwani Serikali inafanya uwekezaji Msimbazi kwa masilahi mapana ya watu wengi.

 "Mtu anakudanganya usisaini kuchukua fidia hiyo, wakati yeye alishasaini siku nyingi, mkitaka niwataje nitawataja. Kwa hiyo,jambo alilolizungumza mtaalamu ni kwamba sasa Mheshimiwa Waziri kwa kuwa wewe huko jikoni unaweza pengine ukatamka kaneno kamoja na roho hizi za wananchi zikapona,"amefafanua Mheshimiwa Chalamila.

Waziri Mchengerwa tena


Aidha, Waziri Mchengerwa amehitimisha suala hilo kwa kubainisha kuwa, Serikali italipa fidia kwa wananchi wote waliokubali kulipwa na kufanyiwa uhakiki wa taarifa zao za kibenki ili kupisha utekelezaji wa mradi huo na tayari Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha kwa ajili hiyo.

"Nimekuja leo kutoa tamko ya hatua ya uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi uanze mara moja kuanzia sasa na hii iende sambamba na ulipaji wa fidia kutokana na tathmini iliyofanywa na wataalam.

"Ninatambua kabisa wapo wananchi asilimia 92 kati ya wote wanatakiwa kulipwa fidia wanasubiria fedha zao na sikatai wapo wengine wenye malalamiko, wataalam wangu endeleeni kuyafanyia kazi na mkishindwa yaje kwangu nione hatua ya kuchukua.

"Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amesema hapa katika misingi ya ukaaji kwenye maeneo wa hatarishi, sheria inaondoa ulipaji wa fidia kwa wakazji wa maeneo hayo.

"Lakini, Mkuu wa Mkoa na waheshimiwa madiwani wamewaombea na kusema hili haliwezekani wananchi wetu tunaomba walipwe hata kifuta jasho, na mimi nikazungumza na Mheshimiwa Rais na akaridhia kila mmoja alipwe kifuta jasho cha shilingi milioni nne."amesisitiza Waziri Mchengerwa.

Baada ya uamuzi huo wa Serikali, wananchi wameonekana kuridhia hatua hiyo na wanatarajia kupokea fedha hizo kwa ajili ya kuondoka katika maeneo hayo ambayo ni hatarishi kwa maisha yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news