DCEA yaendelea kuwamulika wasanii, watu wanaohamasisha dawa za kulevya

DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema, msanii au mtu yeyoye atakayehamasisha matumizi ya dawa za kulevya nchini atawajibishwa kwa mujibu wa sheria yao.

Hayo yamebainishwa Novemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenenerali wa DCEA, Aretas Lyimo katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Runiga ya ITV ambapo aliangazia mambo mbalimbali kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini.

"Hii kauli tuliyoitoa kwamba, wasanii wanaotumia dawa za kulevya tutachukua hatua, msanii katika muktadha anatoa ujumbe kwa jamii, msanii ni kioo cha jamii.

"Sasa, msanii kama ni kioo cha jamii, kile anachokitoa kwa jamii mara nyingi huwa kinapokelewa kwa uzito mkubwa na rika zote, kuanzia watoto mpaka watu wazima.

"Na mara nyingi tunawaona wasanii, wanapotoa hata nyimbo zao, jumbe mbalimbali wanazozifikisha kwa jamii mara nyingi zinapokelewa kwa uzito na kwa ukubwa.

"Sasa, kama msanii ni kioo cha jamii, ndiyo maana tumelenga zaidi kwa wasanii kwamba, msanii yeyote kuanzia sasa hivi atakayetunga nyimbo yoyote inayohamasisha matumizi ya dawa za kulevya, atakayevaa mavazi yanayohamasisha matumizi ya dawa za kulevya, lakini matendo na maneno yake ambayo yanahamasisha matumizi ya dawa za kulevya tutachukua hatua.

"Na sheria inaturuhusu kufanya hivyo, na ninazungumza nikijiamini kabisa kwamba lazima tutafanya hivyo, ili tuijenge jamii yetu, katika kuijenga jamii yetu, katika kuilinda jamii hatupaswi kuogopa.

"Hatupaswi kumuogopa mtu bila kujali umaarufu wake, bila kujali ukubwa wa mtu, lazima tuhakikishe kwamba yeyote yule ambaye anaiharibu jamii, lazima tuhakikishe kwamba, tunachukua hatua.

"Na sheria ipo, na sheria inaturuhusu na ndiyo maana tumewaomba na kuwapa muda kwamba, wasanii wote wasikie huu ujumbe, kwamba kwa kuwa wao ni kioo cha jamii tunawaomba watoe jumbe zinazoijenga jamii, jumbe zinazoleta maadili kwa jamii.

"Lakini, pia nyimbo watakazokuwa wanatunga sasa hivi, zihamasishe watu kuacha matumizi ya dawa za kulevya ili tuijenge jamii yetu, tuijenge Tanzania ambayo ina maendeleo endelevu ina jamii yenye tabia njema, yenye maadili na siku zote hata Serikali inasisitiza kwamba, lazima tuhakikishe tunajenga jamii yenye maadili.

"Unapoleta maendeleo endelevu kama jamii maadili hayapo, yale maendeleo yanaweza yasiwe na maana, kwa hiyo lazima tuhakikishe kwamba tunasisitiza kwenye maadili na huko baadae masuala mengine yakiwemo ya maendeleo yataendelea vizuri.

"Kwa hiyo nitoe wito kwao, na nitoe msisitizo mkubwa kuhusu hili jambo kuwa ni lazima, sheria inaturuhusu na tutafanya hivyo, kwamba yeyote na siyo wasanii tu, yeyote yule ambaye atafanya vitendo vinavyohamasisha matumizi ya dawa za kulevya tutachukua hatua.

"Na tumelenga zaidi wasanii kwa sababu, wao wanapeleka jumbe zaidi kwa wananchi na zinapokekelewa kwa uzito mkubwa sana, kwa hiyo tuwaombe waache kutumia na kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya, na si kuhamasisha matumizi ya dawa za kulevya,"amefafanua kwa kina Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Wakati huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka hiyo ina orodha ambayo inahusisha watu mbalimbali wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya wakiwemo wasanii.

"Sasa, ile orodha tutaanza kuifanyia kazi,lakini pia kuna watu mbalimbali ambao tunawakamata ambao wana wanakuwa wanauza dawa za kulevya, mara nyingi tunapowakamata lazima tuwahoji, kabla ya kuwapeleka mahakamani lazima tuwahoji, ili kujua je? Hizi dawa unazouza, watu unaowauzia ni kina nani.

"Kwa hiyo, wengine wanawataja wale watu ambao wanawauzia, na kuna mtu mkubwa sana ambaye tumemkamata ambaye ni mfanyabiashara mkubwa wa dawa za kulevya na ametaja baadhi ya watu ambao anawauzia wakiwemo wasanii.

"Sasa, zile taarifa tunazichukua tunazifanyia uchunguzi, tunavyozifanyia uchunguzi baadae tunathibitisha kwa matendo ya yule mtu, maneno yake na pengine uhamasishaji wake kwa jamii juu ya matumizi ya dawa za kulevya, kwa hiyo mwisho wa siku tutamuita, tutamuhoji na baadae ili kuthibitisha tutampima.

"Tukishathibitisha kwamba,anatumia dawa za kulevya pia sheria inaturuhusu kumpeleka mahakamani na Mahakama kulingana na vile vipimo vya kisayansi itatoa huku, na kifungo chake kwa mujibu wa sheria yetu ni faini ya shilingi milioni moja au miaka mitatu jela, au vyote viwili.

"Na, pale kulingana na majibu ya vipimo kama itathibitika tayari amekuwa mrahibu anahitaji tiba, basi Mahakama inaamua apewe tiba akiwa ndani ya gereza au apewe tiba akiwa nje ya gereza kulingana na hali yake itakavyokuwa,

"Kwa hiyo tunafanya haya kwa mujibu wa sheria, na wala si tu kwamba mtu anaibuka anatamka hayo maneno, ni kwa mujibu wa sheria na Sheria imetungwa na Bunge na imepitishwa na Bunge na tutahakikisha kwamba, tunatimiza hiyo sheria.

"Na katika kutimiza hiyo sheria, hatuna haja ya kuogopa kwa sababu lazima tuhakikishe kwamba tunataka tuijenge jamii isiyotumia dawa za kulevya, na siyo kiki wala nguvu za soda.

"Kwa hiyo, tuwahakikishie Watanzania hili tutalifanya na kwa wale wote ambao watakuwa wanasisitiza na kuhamasisha dawa za kulevya na siyo wasanii tu wote, kwa hiyo wasikie huu ujumbe na tutahakikisha Tanzania inakuwa salama na inaendelea kutokuwa na matumizi ya dawa za kulevya, hilo nilitoe kwa msisitizo mkubwa sana na waelewe,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news