DCEA yatoa msimamo udhibiti wa bangi nchini

DAR ES SALAAM-Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo amewataka wanasiasa ambao wanakejeli operesheni zinazofanyika kuteketeza na kutokomeza kilimo cha bangi nchini kuacha, kwani dawa za kulevya zina madhara kijamii, kiafya, kiuchumi na kisiasa.

Ametoa wito huo Novemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Runiga ya ITV ambapo aliangazia mambo mbalimbali kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini.

"Mimi nitoe wito kwao, bangi zina madhara makubwa na ni sheria, na sheria pia imetungwa na Bunge na imepita bungeni kwamba tukataze dawa za kulevya aina ya bangi na zisitumike kabisa Tanzania.

"Lakini, ukiangalia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambacho ndiyo chama tawala kinachoongoza Tanzania sasa hivi, chini ya Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwenye ilani yao imeweka msisitizo, kwenye ilani yao sura ya 1 kipengele J wakakisome.

"Kimeweka msisitizo kabisa kwamba kwenye ilani lazima wahakikishe pamoja na mambo mengine,wanaweka juhudi kuhakikisha kwamba uzalishaji, usambazaji, matumizi na aina yoyote ya dawa za kulevya nchini inakomeshwa.

"Kwa hiyo na sisi (DCEA) tunafanya kazi kupitia ilani kwa sababu wote tunaongozwa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.

"Lakini, pia pamoja na hilo ipo sheria ambayo imetungwa na Bunge kwamba dawa za kulevya aina ya mirungi kwa namna yoyote ile zisizalishwe, zisisambazwe na zisitumiwe na mtu yeyote nchini Tanzania.

"Lakini, pia kwenye Jedwali la Kimataifa na yenyewe himo, kwamba bangi hairuhusiwi, kwa hiyo wale ambao wanakejeli au wanazungumza, mimi ninatoa wito kwao, wao pia ni kioo cha jamii wahakikishe wao ndiyo wanatoa maelekezo kwa jamii.

"Lakini, wao ndiyo wanatakiwa watekeleze yale waliyokubaliana au waliyopitisha kwamba sisi haturuhusu kilimo cha bangi, haturuhusu matumizi ya bangi kwa sababu yana madhara kwa afya,lakini ukiachilia madhara kwa afya yana madhara kwa usalama wa nchi.

"Kwa sababu, wanaotumia bangi mara nyigi ndio wanaofanya fujo, ndio vibaka, lakini pia ina madhara kiuchumi kwa sababu hakuna mgeni au mwekezaji atakayewekeza sehemu ambayo hakuna usalama.

"Kwa hiyo, yote haya yana madhara kiuchumi, lakini pia ya madhara kisiasa pia, kwa sababu wale watu wanaovuta bangi wale, ukiwa-mobilize unaweza kuwatumia kwa matumizi mabaya ya kuandamana, kuleta fujo na kupora mali za watu.Mtu wa kawaida ambaye hatumii dawa za kulevya hawezi kufanya yale matendo,"amefafanua kwa kina Kamishna Jenerali, Lyimo.

Amesema, bangi kwenye sheria za Tanzania ni kati ya dawa za kulevya ambazo zimekatazwa kuanzia kilimo, kuziuza na hata kuzitumia.

"Kwa hiyo, mpaka sasa hivi sheria yetu inatambua bangi ina madhara makubwa kwa jamii, lakini pia hata wanasayansi wataalam wa afya wamethibitisha kwamba bangi ina madhara makubwa, nenda kwenye hospitali kwa sababu watu wengine wakati mwingine wanazungumza bila takwimu.

"Lakini,ukienda kwenye hospitali zetu, matatizo ya akili yanaongezeka kutokana na matumizi ya bangi na bahati nzuri siku hizi kuna vipimo vya kisasa kabisa, ukipima unajua huyu mtu ameathirika kwa sababu ya dawa za kulevya aina gani.

"Na ukijaribu kuangalia dawa nyingi ambazo zinatumiwa Tanzania ni bangi na bangi inasababisha sana matatizo makubwa ya akili na ndiyo maana zimekatazwa, lakini pia kidunia pia bangi ipo kwenye jedwali la dwa za kulevya.

"Na imekatazwa kisheria kwamba, haifai kwa matumizi ya ya kuvuta au kutumia na ipo wazi kabisa, kwa hiyo hata kikao tulichofanya mwezi wa nane kule Nigeria ambacho kilijumuisha wakuu wa vyombo vyote vya kupambana na dawa za kulevya Afrika na Dunia kwa ujumla, bangi ni sehemu moja wapo ambayo ilizungumziwa sana kwamba ina madhara makubwa sana kwa jamii.

"Kwa sababu wale wavutaji wa bangi asilimia kubwa inaathiri ubongo, inaathiri uwezo wao wa kufikiri, inaathiri uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi, kwa hiyo inasababisha anafanya matendo ambayo siyo ya kawaida siyo ya kibinadamu na katika jamii eneo lolote ambalo linakuwa na ukithiri wa wa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi uhalifu katika lile eneo unakuwa juu.

"Kwa nini uhalifu unakuwa juu? Kwa sababu bangi inahamasisha pia matendo yasiyofaa, inahamasisha uhalifu, kwa hiyo ndiyo maana tunakataza matumizi ya bangi, lakini pia tetezi zinaendelea kuwa bangi ni uchumi.

"Huo, uchumi wanaouzungumzia hauwezi kulingana na hasara inayotokea, unaweza pia ukaruhusu hicho kilimo cha bangi, ndiyo, lakini faida utakayoipata na hasara utakayoipata ukilinganisha hasara ni kubwa kuliko faida.

"Kwa hiyo, sisi kama Tanzania mpaka sasa hivi msimamo wetu haturuhusu kilimo cha bangi na ndiyo maana tunafanya operesheni maeneo yote na tunawaasa Watanzani wote wale ambao wanaendelea na kilimo cha bangi waache maana operesheni tunazozifanya zinafika kila eneo ambalo linazalisha zao la bangi."amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news