DCEA:Mirungi ina madhara kiafya, ajali

DAR ES SALAAM-Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA),Aretas Lyimo amesema, dawa za kulevya ina ya mirungi zina athari kubwa kiafya na ni chanzo cha ajali nyingi barabarani.

Ameyasema hayo Novemba 20, 2023 jijini Dar es Salaam katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na Runiga ya ITV ambapo aliangazia mambo mbalimbali kuhusu tatizo la dawa za kulevya nchini.

"Kwetu sisi Tanzania, mirungi ni dawa za kulevya, lakini pia katika ile orodha ya Kimataifa kwenye jedwali mirungi himo, ni moja wapo ya dawa ambazo pia zina athari kubwa kwa afya ya jamii kwa watumiaji hususani inaleta magonjwa mengi, saratani ya koo,saratani ya tumbo lakini na magonjwa mengine ambayo yanamuathiri yule mtumiaji.

"Lakini, pia kwenye nchi yoyote duniani, kila nchi ina sera zake ina namna inavyoongoza nchi kulingana na taratibu zao walivyojiwekea.

"Kwa hiyo, Kenya wao kulingana na sera zao, wamejiwekea kwamba mirungi waitumie kama ni zao la kiuchumi, lakini kwetu sisi Tanzania mirungi bado hatujairuhusu kama zao ambalo linaruhusiwa kutokana na kwamba, madhara yake makubwa yanatokana na matumizi ya mirungi hususani madhara ya kiafya zaidi.

"Lakini, pia ajali zinazotokea barabarani, kwa wale wanaotumia mirungi, kwa sababu mirungi yenyewe asili yake inaondoa usingizi, lakini pia ile kemikali yake ikishaisha usingizi unakuja kwa ghafla.

"Kwa hiyo ndiyo unajikuta hata dereva anayetumia mirungi, mwisho wa siku usingizi unakuja ghafla unashangaa dereva amepata ajali eneo ambalo siyo la kupata ajali, ni kutokana na hizo athari za matumizi ya mirungi.

"Kwa hiyo sisi sera yetu kama Tanzania haturuhusu mirungi,tumefanya operesheni kubwa Kilimanjaro, tumekamata shehena kubwa ya mirungi pale ambayo imetoka Kenya inaingia Tanzania.

"Kwa hiyo hata Wakenya tumeshazungumza nao kwamba tutaingia nao upya makubaliano ya kufanya operesheni za pamoja, kuhusiana na dawa za kulevya aina za viwandani, lakini pia hizi za mashambani, kwamba wao kama kule kwao wameruhusu mirungi itumike, lakini wao pia watusaidie wasiruhusu iingie Tanzania.

"Kwa hiyo kuna MoU tunaiandaa na tutafanya nao makubaliano, kufanya operesheni za kushirikishana, lakini pia nchi zote za Afrika Mashariki ikiwemo Uganda, Malawi, Zambia, Msumbiji, Afrika Kusini na maeneo mengine yote tumeshakubaliana kuwa tutaingia nao mkataba.

"Tayari Afrika Kusini tumeingia nao mkataba ili kuhakikisha kwamba tunashirikiana katika operesheni za kudhibiti dawa za kulevya, Msumbiji tayari tumeshaingia nao mkataba.

"Zambia ndiyo sasa hivi tuko nao kwenye MoU tumeshaandaa sasa hivi iko kwenye mamlaka za kisheria ili kuipitia na kuona kwamba imekaa vizuri ili tuweze kusainiana mkataba.

"Kenya ndiyo tuko kwenye hatua za awali pamoja na Malawi. Lengo ni kuhakikisha kwamba, kama mimi sheria yangu hairuhusu dawa hizi kutumika, basi zile nchi zinazozunguka zihakikishe na wao hawaruhusu zile dawa ziingie kwetu.

"Na sisi, haturuhusu pia dawa kutoka huku ziingie kwenye nchi zao, ndiyo hayo makubaliano tutaingia ili kuhakikisha kwamba, tunafanya operesheni za pamoja na tunahakikisha kwamba, tunapunguza tatizo la dawa za kulevya katika nchi zetu hizi,"amefafanua Kamishna Jenerali Aretas Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news