Karume Boys watwaa ubingwa CECAFA, shukurani kwa Rais Dkt.Mwinyi

KAMPALA-Juhudi za Serikali ya Awamu ya Nane za kuimarisha sekta ya michezo Zanzibar zimeanza kuonesha matokeo chanya.

Ni baada ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya Zanzíbar kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA U15).

Katika mchezo huo uliofanyika Novemba 16, 2023 Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Njeru jijini Kampala nchini Uganda mtanange ulionekana kuwa wa moto zaidi.

Wakiongozwa na Mohamed Mohamed, timu ya Zanzibar iliilaza Rhinos ya Uganda 4-3 kwa mikwaju ya penalti baada ya mechi hiyo kutoka sare ya 1-1.

Lukman Omar aliifungia Zanzibar bao la kuongoza baada ya dakika 19, lakini Rhinos ya Uganda walijibu mapigo kwa kusawazisha dakika ya 30 kupitia kwa Ibra Ssebagala. Timu hizo mbili zilishindwa kupata mabao zaidi katika kipindi cha pili.

Lakini kipa wa Zanzibar, Mahir Amour ambaye pia alikuwa shujaa walipoitoa Sudan Kusini katika hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penalti, aliibuka na kusimamisha mikwaju miwili ya penalti na kuhakikisha timu yake inashinda 4-3.

”Vijana wamejitahidi sana kuwa mabingwa,”alisema kocha wa Zanzibar, Mohamed Mrishona Mohamed ambaye alionekana kuwa na furaha wakati wote baada ya mechi kumalizika.

Wakati wa tuzo, Owen Mukisa wa Uganda alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora, huku Amour wa Zanzibar akiwa kipa bora.

Lazarus Peter George kutoka Sudan Kusini ambaye alifunga mabao nane aliibuka kuwa mfungaji bora.Hafla ya tuzo hizo ilihudhuriwa na Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Wallace Karia na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Uganda (FUFA), Moses Hassim Magogo.

Timu nane zilizoshiriki michuano hiyo ya kanda ni pamoja na Zanzibar, Uganda, Tanzania, Sudan Kusini, Djibouti, Ethiopia, Rwanda na Somalia.

Miongoni mwa juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane chini ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya michezo.

Jitihada hizo zimerejesha morali kubwa katika soka la Zanzibar ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi ambapo wadau wengi wameanza kuunga mkono michezo na hata kudhamini ligi kuu ya Zanzibar.

Mapema mwaka huu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt. Hussein Ali Mwinyi alisema kwamba Serikali itajenga viwanja vya kisasa vya michezo kila wilaya na mkoa pamoja kuufanyia ukarabati mkubwa Uwanja wa Amani.

Alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi baada ya kuweka jiwe la msingi la uwanja wa michezo unaojengwa Matumbaku.

Rais Dkt.Mwinyi alisema, viwanja hivyo vitajumuisha michezo ya aina mbalimbali ili kutoa fursa pana kwa vijana kuweza kushiriki michezo.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amewapongeza Karume Boys kwa ushindi huo huku akiwatakia kila la heri.

"Hongereni sana Timu ya Taifa ya Soka ya Zanzibar kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 (Karume Boys), kwa kutwaa ubingwa wa CECAFA U15 2023.

"Mmetupa heshima kubwa. Nawatakia kila la kheri katika ndoto na safari yenu kwenye mchezo wa soka siku za usoni,"amebainisha Rais Dkt.Samia kupitia mitandao yake ya jamii.

Mbali na hayo, katika michuano hiyo, Tanzania Bara wamefanikiwa kumaliza nafasi ya tatu kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya Sudan Kusini katika mchezo uliotangulia hapo hapo Uwanja wa Kituo cha Ufundi cha FUFA jijini Kampala.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news