Wakulima wahamasishwa kuzingatia kilimo mseto na kilimo hifadhi

NA FRESHA KINASA

SERIKALI imesema katika kuhakikisha utoshelevu wa chakula unaendelea kuimarika nchini wakulima wana jukumu la kujikita kufanya kilimo mseto na kilimo hifadhi ambavyo vitaweza kuendana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kukabili changamoto mbalimbali za kimazingira hapa nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe kupitia hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Agnes Meena katika Maonesho ya Nane ya Kilimo mseto yanayofanyika katika viwanja vya AICT Bweri vilivyopo Wilaya ya Musoma Mkoa wa Mara.

Maonesho hayo yanafanyika kuanzia Novemba 16, 2023, hadi Novemba 18, 2023 yakienda sambamba na maadhimisho ya miaka ya 40 ya Shirika la Vi-Agforestry katika ukanda wa Afrika Mashariki. Ambapo wadau mbalimbali wa kilimo, ufugaji na uvuvi pamoja na wananchi wanashiriki katika maonesho hayo yakiwa na kauli mbiu isemayo;
"Panapostawi miti-Watu hustawi". Amesema kuwa, sekta ya kilimo ni muhimu sana katika kuhakikisha utoshelevu wa chakula, lakini kumekuwepo na baadhi ya changamoto ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi ni vyema wakulima wakaendana na mabadiliko kwa kulima kisasa na kufuata kanuni na mbinu Bora ikiwemo Kilimo hifadhi na mseto kupata mazao mengi kwa tija.

Prof. Shemdoe amesema, serikali ya Tanzania imeendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kuhakikisha sekta ya Kilimo inazidi kuleta mchango mkubwa kwa maendeleo ya Wananchi na pia serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za mashirika yanayojishugulisha na Kilimo pamoja na kutoa ushirikiano katika kuinua uchumi wa nchi.

Aidha amelipongeza Shirika la Vi-Agforestry kwa mchango wake katika sekta ya Kilimo na uhifadhi wa mazingira kwani hatua hiyo imekuwa na manufaa makubwa na Serikali inathamani jitihada za Shirika hilo na itaendelea kulipa ushirikiano katika kuleta ufanisi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu kutoka Ofisi kuu ya Shirika la Vi- Agroforestry nchini Sweden Charlotta Szszepanowsk amesema kuwa kwa miaka 40 tangu kuwepo kwa Shirika la Vi- Agroforestry katika Ukanda wa Afrika mashariki limeweza kutoa Miche bure kwa wananchi na kufanya kazi kwa kuzingatia haki za binadamu.

Pia amesema kuwa Shirika limeweza kupanda Miti Mil. 156, kuyafanya mashirika ya wakulima kuwa na nguvu na kuboresha maisha ya Wananchi wa Vijijini kupitia Kilimo mseto na Kilimo hifadhi.

Ameongeza kuwa Shirika hilo limeweza pia kushiriki kuboresha usalama wa Chakula na lishe kwa wakulima wadogo, kutoa elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuhifadhi baionaua kwa maendeleo endelevu kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali.

Pia amesema kuwa katika miaka mitano iliyopita wameweza kutekeleza programu ya 'alive' yenye lengo kuu ambalo lilihusu mazingira endelevu na mpango huo na wabia 28 wanaofanya kazi na takribani wakulima 231,000 nchini Tanzania, Uganda Kenya na Rwanda.

Amewaomba Viongozi ndani ya Tanzania na Africa mashariki kuweka kipaumbele kwa mkakati wa kitaifa wa Kilimo mseto kwani ni Msingi wa kuitatua changamoto za wakulima katika Ukanda wa afrika mashariki. Sambamba na kuleta Mapinduzi katika Kilimo.

Amesema mabadiliko ya tabia nchi yanaathiti wakulima hadi Viongozi wanaotekeleza sera za serikali na kwamba matumizi ya ardhi ni muhimu kwa maendeleo ya nchi. Huku Shirika hilo likisema safari ya miaka 40 imekuwa ya kujitolea kwa ajili ya kuinua wakulima.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mosses Kaege akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Halfan Haule amelishukuru Shirika la Vi- Agroforestry kwa kuendelea kuwapa elimu wakulima na kuwapa elimu ya uhifadhi na pia amewaomba Wananchi wa Mkoa wa Mara kutumia msimu huu wa mvua kupanda Miti katika kutunza uoto wa asili.

Mashaka Charles Mkulima kutoka Shirika la BUFADESO la Wilayani Bunda amesema kupitia Kilimo mseto ameweza kupiga hatua kimaisha ikiwemo kuwa na uhakika wa kutosha wa Chakula, kisomesha Watoto wake Hadi elimu ya chuo kikuu, kujenga Nyumba ya kisasa, kumiliki shamba kubwa la miti, na kukidhi mahitaji ya familia yake.

Mchungaji Philipo Kanwelle wa Kanisa la AICT kutoka Shirika la IDS ambalo limekuwa likishirikiana na Shirika la Vi-Agforestry kufanya maeonesho hayo kila mwaka amesema kuwa Shirika la IDS Mkoa wa Mara limeweza kuwafikia zaidi ya wakulima 800 kuwapa elimu ya Kilimo bora na mbinu sahihi za kilimo mseto sambamba na utunzaji wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news