Miaka 36 ya TAMWA, Serikali yasisitiza

DAR ES SALAAM-Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetakiwa kuweka mkazo mkubwa katika uhuru wa kujieleza unaojumuisha sauti za wanawake ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama wakati alipomuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 36 ya TAMWA yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri (Sera, Bunge na Uratibu (Mhe. Jenista Mhagama akipokea tuzo kwa niaba ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyopewa na TAMWA.

Waziri ametoa wito kwa TAMWA kuona umuhimu wa mijadala yenye mlengo wa kijinsia na uhusiano kati ya uhuru wa vyombo vya habari, ulinzi na usalama wa waandishi wa Habari wanawake, na uhuru wa kujieleza kuwa kitovu cha kufanya maamuzi katika ngazi ya jamii kitaifa, na kimataifa.
“Tuadhimishe siku hii kutimiza ahadi zilizotolewa na kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa ili kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yote na hasa lengo namba tano linalozungumzia usawa wa jinsia,” amehimiza.

Aidha, wadau mbalimbali wa habari watumie siku hii kusherehekea kwa kuungana na TAMWA kulinda na kuthamini haki za wanawake, haki za wasichana, haki za watoto, maadili ya kitanzania, na kupinga ukatili wa jinsia majumbani, hadharani na mitandaoni.
“Wamiliki wa vyombo vya habari na waandishi wote kwa ujumla muungane katika jitihada za ulinzi na usalama wa waandishi wa habari wanawake na hapa niwatie moyo waandishi wa Habari wanawake kuwa kazi yenu nzuri inaonekana pale mnapoweka jitihada ya kufanya kazi kwa weledi bila kukatishwa tamaa na vikwazo vya kimazingira,"amefafanua.

Waziri amesema, kama kauli mbiu inavyosema, Uongozi Bora na Mchango wa Wanawake ni Chachu Kuelekea Tanzania yenye Maendeleo endelevu.
Hatuna budi kutambua kwamba suala la jinsia sio suala la wanawake peke yao bali ni suala la kuchochea maendeleo ya taifa letu miongoni mwa wanawake na wanaume, kwani ni jambo linalohimiza ushirikishwaji na ujumuishi usioacha kundi lolote nyuma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw, Selestine Gervas Kakele amesema, Serikali inatambua mchango wa TAMWA na wakati wote serikali itaendelea kuangalia ujumbe ambao TAMWA na asasi nyingine inatoa.
"Tumepokea utafiti kuhusu unyanyasaji wa kijinsia, TAMWA kupitia utafiti huu imesaidia kuvunja ukimya, matokeo ya utafiti hayalengi kunyoosha kidole kwa mtu, bali kushirikiana ili tuweze kuishinda vita hiyo.

“Tusimamie weledi na nidhamu ya kazi na pale vitendo hivi vinapojitokeza: wahanga wasikae kimya jitokezeni, pazeni sauti na serikali itasikia,” alifafanua.
Awali Mwenyekiti wa TAMWA, Bi.Joyce Shebe amemshukuru Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali mwaliko.

“Tumeona jinsi serikali ambavyo inapitia mifumo ya kisera na kisheria ilikuja na mipango inayopimika katika kuhakikisha ushirikishwaji na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na masuala yanayohusu usawa wa kijinsia inatatekelezeka.

"TAMWA tunaahidi kumuunga mkono kivitendo kwa sababu ni jukumu ambalo tumealianza tangu miaka 36 iliyopita."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news