Rais Dkt.Samia aomboleza vifo vya abiria 13 ajali iliyohusisha basi na treni Singida

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan ameelezea kupokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu 13 katika ajali iliyohusisha basi na treni mkoani Singida leo.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ameeleza kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii kuwa, "Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya watu kumi na tatu katika ajali ya basi mkoani Singida mapema leo.

"Natuma salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa ndugu zetu hawa 13 waliotutoka, na tuungane kwa pamoja katika kuwaombea Mwenyezi Mungu awarehemu.

"Tuwaombee pia pona ya haraka majeruhi wa ajali hii katika matibabu yao yanayoendelea kwenye hospitali za Mtakatifu Gaspar, Benjamin Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

"Tumeanza kipindi cha mwisho wa mwaka, naendelea kutoa wito kwetu sote kuongeza umakini katika kuendesha vyombo vya moto, kufuata sheria za usalama barabarani na usimamizi madhubuti,"ameeleza Rais Dkt.Samia.

Katika ajali hiyo ya basi mali ya Kampuni ya Ally's Star na treni iliyotokea alfajiri leo Novemba 29, 2023 mkoani Singida imeua watu 13 na kujeruhi wengine 25.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC), imesema ajali hiyo imehusisha basi la abiria lenye namba T178 DVB mali ya kampuni hiyo kugonga kichwa cha treni chenye namba V951 9006 kilichokuwa kikitokea Stesheni ya Aghondi kuelekea Manyoni katika makutano ya reli na barabara eneo la Manyoni mkoani Singida.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Jamila Mbarouk ameeleza kuwa,“Ajali imehusisha basi la abiria lililokuwa likivuka njia ya reli eneo la kilomita 587 Manyoni na kichwa cha treni na kusababisha majeruhi 25, wanawake 7, wanaume 18 na vifo vya watu 13, wanawake 6, wanaume 7.

"Shirika linatoa pole kwa ndugu wa marehemu na Mwenyezi Mungu awape nafuu majeruhi waweze kuendelea na shughuli za kujenga taifa.”

Taarifa hiyo imesema, TRC itaendelea kuutaarifu umma kadiri taarifa zinavyopatikana na kushauri madereva kuheshimu sheria za barabarani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news