REA yatenga shilingi bilioni 10 kusambaza mitungi ya gesi vijijini

NA VERONICA SIMBA
REA

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), katika Mwaka huu wa Fedha (2023/24), umetenga shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kusambaza mitungi ya gesi ya LPG, majiko na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini kwa njia ya ruzuku.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia), akiwasilisha Taarifa ya Utendaji Kazi wa Wakala hiyo kwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga (katikati), Novemba 7, 2023. Naibu Waziri alitembelea Makao Makuu ya REA jijini Dodoma na kuzungumza na Menejimenti ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka.

Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy ameyasema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya Wakala kwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, Novemba 7, 2023.

Alisema kuwa, kiasi cha mitungi kati ya 200,000 hadi 500,000 inatarajiwa kusambazwa katika maeneo ya vijijini kutegemea kiwango cha ruzuku kitakachotolewa.
Mitungi yenye majiko ya gesi ikiwa imeandaliwa tayari kwa kugawiwa kwa umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Ruvuma hivi karibuni ikiwa ni Mpango maalumu wa uwezeshaji wanawake waishio vijijini kutumia nishati safi ya kupikia. Uwezeshaji huu kwa njia ya ruzuku unatolewa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akielezea Mradi wa usambazaji gesi ya kupikia kwa ujumla, Mhandisi Saidy alisema unategemewa kusambaza mitungi ya gesi 70,020 ambapo hadi kufikia Agosti 15 mwaka huu, mitungi 23,806 (sawa na asilimia 34) ilikuwa imeshasambazwa kwa wananchi mbalimbali kupitia kwa Wabunge ambao ni wawakilishi wao.

“Lengo la Serikali kupitia REA katika utekelezaji wa Mradi huo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika maeneo yao,” alifafanua.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu alieleza kuwa, katika hatua nyingine, REA inatekeleza Mradi wa usambazaji gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Lindi na Pwani kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), ambapo alisema Mkataba umesainiwa na maombi ya fedha za awali, yapo Wizara ya Fedha kwa ajili ya uhakiki. Naibu Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge anayewakilisha Vijana Mbinga, Judith Kapinga akiwasha jiko la gesi muda mfupi kabla ya kugawa majiko hayo kwa umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni. Mheshimiwa Kapinga aligawa majiko hayo ikiwa ni sehemu ya Mpango Maalumu wa Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuwawezesha wananchi wa vijijini kupitia Wabunge wao, kutumia nishati safi ya kupikia.

“Mkataba huu una jumla ya shilingi bilioni 6.8 ambapo unatarajiwa kuunganisha wananchi 980 na nishati ya kupikia katika maeneo ya Mnazi Mmoja mkoani Lindi na Mkuranga mkoani Pwani.”

Alisema kuwa, katika Mwaka huu wa Fedha (2023/24), REA imetenga shilingi bilioni 18.5 kwa ajili ya kuiwezesha TPDC kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia katika maeneo yaliyopo pembezoni mwa Mkuza wa Bomba Kuu la kusafirisha gesi asilia linalopita katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani ili wananchi wanaoishi kwenye maeneo hayo waweze kutumia gesi asilia kwa ajili ya kupikia.

Mkurugenzi Mkuu pia alieleza kuhusu Mradi wa ufungaji mifumo ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300 ambapo alisema Wakala unalenga kujenga mifumo hiyo kwa Taasisi 100.

Akifafanua, alisema kuwa Mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati akifungua Kongamano la Nishati ya Kupikia jijini Dar es Salaam, Novemba 2022.

Baadhi ya wafanyakazi wanawake wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakiwa katika picha ya pamoja. Wanawake hawa wamejiwekea utaratibu wa kuchanga fedha na kununua majiko na mitungi ya gesi ambapo hugawa katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwawezesha wanawake waishio vijijini kutumia nishati safi ya kupikia.

Kuhusu usambazaji wa majiko banifu, alieleza kuwa kupitia ruzuku ya Dola za Marekani milioni sita iliyotolewa na Benki ya Dunia, Serikali kupitia REA inatarajia kusambaza majiko banifu 70,000 yaliyotengenezwa kwa teknolojia yenye ubunifu wa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa pamoja na kupunguza uharibifu wa mazingira.

Naibu Waziri Kapinga alitembelea Makao Makuu REA jijini Dodoma na kuzungumza na Menejimenti yake ikiwa ni mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news