Serikali yawekeza mitambo 142 kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) imesema kuwa, katika mwaka 2021/22 Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa wa mitambo ya kisasa na vifaa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 30, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt.Fidelice Mafumiko katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambapo mitambo 142 inajumuisha mikubwa na midogo.

"Eneo la pili ambalo tumeona katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita limekuwa na mafanikio ni uwekezaji katika ununuaji wa mitambo na vifaa vya kisasa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.
Afisa Uhusiano Mwandamizi, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), Bw. Sabato Kosuri, akiongoza kikao hicho.

"Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 Serikali imeweza kununua mitambo mikubwa minane na midogo 134 ambayo thamani yake kwa ujumla ni shilingi bilioni 9.3.

"Hii ni mitambo ambayo imewekwa kwenye maabara zetu zilizoko Dar es Salaam, zilizoko pia Arusha, zilizoko Mwanza na kwa sasa ambayo inaendelea kusimikwa kwenye jengo letu la Dodoma.
"Tunaamini kupitia uwekezaji huu kwenye mitambo, utaongeza kasi ya utoaji huduma hasa za uchunguzi wa kimaabara na na kutoa matokeo kwa wakati, lakini na kuwafikia wananchi walio wengi,"amefafanua Mkemia Mkuu.

Mamlaka ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na.8 ya Mwaka 2016.

Pamoja na majukumu mengine, Sheria ya Mamlaka inaipa jukumu mamlaka ya kuwa chombo cha juu na Maabara ya Rufaa katika masuala yote yanayohusu uchunguzi wa sayansi jinai na huduma za vinasaba, ubora wa bidhaa na usimamizi wa kemikali.

Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imepitia mabadiliko mbalimbali kutoka kuwa idara ndani ya wizara, wakala kati ya mwaka 1999-2016 na kuwa mamlaka kuanzia tarehe 5 Aprili,2017 hadi sasa.

Aidha, kihistoria mamlaka hii ilianza kama kituo cha kufanya utafiti wa magonjwa ya ukanda wa joto kwenye maabara ya taifa mwaka wa 1895 na baadae kuhamishiwa Wizara ya Afya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mwaka 1947.

Kati ya mwaka 1947-1959 maabara ilihamishiwa Wizara ya Kilimo na Maliasili na kutoka mwaka 1958 hadi sasa maabara ipo chini ya wizara yenye dhamana ya afya nchini.

Vile vile, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeimarisha utekelezaji mzuri wa majukumu yake, kufikiwa kwa malengo, dhima na dira yake, hivyo kuchangia jitihada za Serikali katika kuboresha ustawi wa watu wake na mazingira.

Katika hatua nyingine, Mkemia Mkuu wa Serikali amesema, "Kuna miradi inaendelea, kuna miradi hii ambayo kati ya sasa 2023/26 inaweza kuwa imekamilika moja ni ujenzi wa ofisi na maabara katika kanda yetu ya Kusini.

"Mamlaka yetu katika utoaji wa huduma zake iko Dar es Salaam, sehemu ya makao makuu ofisi ndogo, lakini na Dodoma vile vile tunatoa huduma kupitia ofisi zetu za kanda.

"Kwa upande wa Kanda ya Kusini ofisi zetu zipo mjini Mtwara, na hapa tuna mradi wa ujenzi ambao tunategemea ukikamilika utatoa huduma kwa mikoa ya Kanda ya Kusini, na pia katika Kanda ya Kusini pia tumepanga tukikamilisha ujenzi wa jengo la Mtwara tunaamini utaondoa gharama kwa Serikali kwa ajili ya upangaji.

"Mradi mwingine ni ujenzi wa ofisi ya Kanda yetu ya Mashariki kwa maana ya Dar es Salaam, Kanda yetu ya Mashariki pamoja na kutoa huduma kule bandarini bado inatumia baadhi ya vioski vidogo vidogo vya toka enzi za enzi.

"Kwa hiyo tuna mradi wa jengo ambao tunategemea utasaidia sana shughuli za kanda na kanda hii ni kubwa, ikihudumia Dar es Salaam na Pwani."

Pia amesema, wana mradi mwingine wa ujenzi wa ofisi na maabara kwenye Ukanda wa Ziwa . "Kanda ya Ziwa hii, ofisi zetu ziko Mwanza lakini inahudumia mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Shinyanga, Mara, Simiyu, Geita, Kagera na Kigoma, kwa hiyo bado hii ni kanda kubwa, kwa hiyo tuna miradi pia inayoendelea."

Miongoni mwa majukumu ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kama yalivyoorodheshwa chini ya Sheria ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya Mwaka 2016 ni kufanya shughuli za utafiti, uchunguzi wa maabara.

Sambamba na kutoa ushauri kwa Serikali kwenye masuala yanayohusiana na uchunguzi wa sayansi jinai toksikolojia, sayansi jinai baiolojia na vinasaba, sayansi jinai kemia, vyakula, dawa usalama mahali pa kazi, kemikali za viwandani na bidhaa zake na sampuli za mazingira kwa ajili ya kutekeleza afua za afya, sheria, ustawi wa jamii na mazingira.

Pia, kuanzisha, kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa Kanzidata ya Taifa ya Vinasaba vya Binadamu kwa mujibu wa Sheria ya Vinasaba, Sheria ya Mamlaka na Sheria.

Majukumu mengine ni kuratibu Programu za Taifa za usimamizi wa kemikali, sayansi jinai na huduma za vinasaba na kusimamia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Sumu.

Katika hatua nyingine, mamlaka inawajibika kusimamia na kuendesha mafunzo na programu za Elimu kwa Umma katika masuala yanayohusiana na usimamizi wa kemikali, huduma za vinasaba na masuala mengine yanayosimamiwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Na. 8 ya mwaka 2016.

Nyingine ni kutengeneza na kutoa mwongozo, maelekezo,fursa, mafunzo na kuwaandaa wanasayansi ndani na zaidi ya utaalam wa majukumu ya mamlaka na kukusanya kutambua na kuchunguza kisayansi vielelezo vinavyohusiana na masuala ya kisheria.

Mamlaka pia inasajili, kusitisha au kufuta maabara za kemikali, sayansi jina na vinasaba vya binadamu, kusitisha au kufuta kemikali za viwandani, kemikali za majumbani au wadau wa kemikali ikiwemo kufuta vibali vya utafiti au leseni za vinasaba.

Aidha, mamlaka hii inawajibika kubatilisha na kutoa maelekezo au uteketezaji wa vitu, kemikali na mazao ya kemikali na kumshauri Waziri kuhusu uteuzi wa wakaguzi, maafisa uchukuaji sampuli na wachunguzi wa maabara wa serikali na mengineyo.

Ofisi ya TR

Akizungumzia kuhusiana na vikao kazi hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR),Thobias Makoba amesema kuwa,
"Huu ni mwendelezo wa vikao vyetu kazi, sisi kama wanahabari na taasisi ambazo Msajili wa Hazina anazisimamia, malengo ni yale yale kuhakikisha umma wa Watanzania unafahamu nini hizi taasisi ambazo ziko chini ya Msajili wa Hazina ambaye anazisimamia kwa niaba ya Serikali, taasisi hizi zinafanya nini.

"Unaowaona hapa wanawakilisha sehemu ya wanahabari Tanzania, wahariri wanakuja hapa kwa malengo mawili, kwanza kujifunza kwa sababu elimu haina mwisho, kufahamu taasisi zinafanya nini.

"Lakini, kupitia uelewa wao ndiyo wanatusaidia umma wa Watanzania kujua nini ambacho hizi taasisi zinafanya, maendeleo ya taasisi hizi, lakini pia na mafanikio ambayo yamefikiwa mpaka sasa.

"Kwa sababu Serikali inavyozidi kupambana kila siku kwa mipango yake ni wajibu wa Serikali kuufahamisha umma maendeleo na mafanikio ambayo taasisi hizo zinafanya."

Amesema, Mamlaka ya Mabaara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (MMS) ni miongoni mwa taasisi ambazo si za kibiashara ikizingatiwa kuwa Msajili wa Hazina anasimamia taasisi za aina mbili kwa maana ya zile ambazo zinafanya biashara na zile ambazo hazifanyi biashara zinatoa huduma kwa jamii.

Makoba amesema,moja ya mashirika au taasisi za kimkakati ambazo zitaendelea kutoa huduma ni Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

""Kwa nini eneo la kimkakati? Mkemia Mkuu yeye anaweza asilete faida ya fedha, lakini mmesikia kwenye utangulizi hapa, kuna maeneo matatu yamekuwa yakijirudia kwanza afya na ustawi wa jamii.

"Taifa ambalo halina afya, wote tunajua afya ndiyo kila kitu, tumeweza kufika hapa kwa sababu tumehamka salama, tumeweza kufika hapa kwa sababu tumekula vyakula ambavyo havina sumu, tumeweza kufika hapa kwa sababu jamii zetu zimelindwa kimwili na kisaikolojia.

"Moja ya kazi ambayo anaifanya Mkemia Mkuu ni kuhakikisha afya za Watanzania ziko salama. Pili kwenye kusimamia sheria na haki,kwa hiyo hata bila ya kuleta faida lakini tuna faida ya kupata haki kwenye jamii ya Watanzania.

"Lakini, tatu mazingira. Tumezungukwa na sumu za kila aina katika maisha yetu ya kila siku, anayetusimamia kuhakikisha tunajua hapa kuna sumu hapa hakuna sumu ukiacha mashirika mengine kama NEMC ni Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

"Kabla bidhaa hazijaingia, hazijatumika nani anatoa leseni, wanaosimamia kuhakikisha wanatoa endorsement ni Mkemia Mkuu wa Serikali, sasa tukasema ni muhimu na yeye apate wasaa wa kutueleza nini katika hayo maeneo anayoyafanya, amefikia wapi, faida yake kwa umma wa Watanzania na mipango yake huko mbele katika kuchangia maendeleo ya Tanzania,"amefafanua Makoba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news