Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu

NA LWAGA MWAMBANBE

NOVEMBA 12, 2023 Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt.Said Mohamed alisema kuwa, kuanzia Novemba 13 hadi Novemba 30, 2023 jumla ya watahiniwa 572,338 watafanya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne.

Katibu Mtendaji huyo alifafanua kuwa, kati ya watahiniwa hao 543,386 ni wa shule na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,952.

Aliyabainisha hayo wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam ambapo katika watahiniwa wa shule 543,386 waliosajiliwa wavulana ni 250,237sawa na asilimia 46.05 na wasichana ni 293,149 sawa na asilimia 53.93.

Vile vile, kwa mujibu wa Katibu Mtendaji huyo watahiniwa wa shule wenye mahitaji maalum ni 614 ambapo kati yao 283 ni wenye uoni hafifu, 24 ni wasioona, 135 wenye ulemavu wa kusikia.

Aidha, 11 ni wenye ulemavu wa akili na 161 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili. Kwa mwaka huu inaonekana kuwa, kuna ongezeko la watahiniwa 8,633 sawa na asilimia 1.61 ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa mwaka 2022 ambao walikuwa 524,753.

Huku kwa watahiniwa wa kujitegemea 28,952 walisajiliwa kati yao wavulana walikuwa ni 11,867 sawa na asilimia 40.99 na wasichana ni 17,085 sawa na asilimia 59.01.

Kwa upande wa wenye mahitaji maalum kwa wanafunzi wa kujitegemea walikuwa nane kati yao wwenye uoni hafifu walikuwa wanne na wasioona wanne.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, subira yavuta heri kwani mwwenye kuvumilia ndiye atafaidi matunda mema ya uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na Serikali katika Sekta ya Elimu kuanzia vijijini hadi mijini. Endelea;


1. Enyi kidato cha nne, mitihani imekwisha,
Sasa nyumbani wanene, mnayo nusu maisha,
Matokeo myaone, mzidi jielimisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

2. Nyie bado ni watoto, msije mkachemsha,
Mjione na mvuto, kwanza muanze maisha,
Kufanya hivyo utoto, tena mwajihangaisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

3. Mna miezi kadhaa, homu mwajipumzisha,
Muache kukaakaa, bila kujishughulisha,
Itakuwa ni balaa, jinsi mtajikausha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

4. Ushauri huu pokea, msikae kujichosha,
Somasoma endelea, akili kuchangamsha,
Ujuzi mpya pokea, ndivyo wajitambulisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

5. Mnapokuwa nyumbani, fanya kupachangamsha,
Usafi wa nje ndani, fanya safishasafisha,
Wazazi toka kazini, mwaweza wafurahisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

6. Mjini na vijijini, mwaweza jishughulisha,
Asubuhi na jioni, mfanye yanayotosha,
Hata wakija wagemni, muweze kuwaridhisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

7. Kazi za mikono pia, nadharia imekwisha,
Nguvu za kwenu tumia, ndiko kujielimisha,
Kesho zitasaidia, mkiyaanza maisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

8. Dunia kidigitali, kweli inafurahisha,
Uwe karibu na mbali, utakacho wafikisha,
Vema tumia akili, yale mnayojilisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

9. Kuikumbatia simu, nayo kujishughulisha,
Ya kwamba unayo hamu, muda wote kuchatisha,
Unajiua fahamu, hata kujichelewesha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

10. Mitandao kutumia, haki hiyo inatosha,
Ni vipi unatumia, vema kujilinganisha,
Unaweza kuumia, ama kujiimarisha
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.

11. Bado ninyi wanafunzi, sasa mwajipumzisha,
Msifanye upuuzi, hata mkajiangusha,
Maadili muyanzi, pema yatawafikisha,
Sikimbilie maisha, kukatisha ndoto zenu.
 
Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news