Tanzania mwenyeji wa Kongamano la Pili la AfCFTA la Wanawake katika Biashara

DAR ES SALAAM-Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa wanawake wa Tanzania kushiriki Kongamano la Pili la Wanawake katika Biashara chini ya Mkataba wa eneo huru la Biashara Afrika ( AfCFTA) litakalofanyika tarehe 06 hadi 08 Disemba, 2023 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam kwa kujisajili kupitia anuani ya tovuti hii https://au-afcfta.org/wit/ au Tovuti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo ni www.viwanda.go.tz
Ameyasema hayo leo Novemba 29, 2023 alipokuwa akiongea na waandishi wa habari katika ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam kuhusu kongamano hilo linaloongozwa na kauli mbiu isemayo "Kuimarisha Ushiriki wa Wanawake katika Biashara na Kuongeza Kasi ya Utekelezaji wa AfCFTA”.
Kongamano ambalo linaandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Sekretarieti ya AfCFTA ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji.

Vilevile, amebainisha kuwa kongamano hilo linalenga kuwakutanisha pamoja wanawake katika biashara kujadiliana, kubadilishana uzoefu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika biashara ili kuwawezesha kuweka mikakati ya kuimarisha ushiriki wao kwenye biashara ndani ya Afrika chini ya Mkataba wa AfCFTA.

Sambamba na kuwawezesha kunufaika ipasavyo na fursa za biashara zinazopatikana na Mkataba wa AfCFTA ili kuongeza ajira na kukuza uchumi imara kwa Taifa na jamii kwa ujumla.

“Wanawake ndio kiini cha biashara na wamekuwa chachu muhimu katika maendeleo ya uchumi duniani, hivyo wanatakiwa kujumuishwa ili kuchangamkia fursa zinazotolewa chini ya mkataba huo,"amesema Dkt. Kijaji.

Akizungumuzia kuhusu washiriki wa kongamano hilo amesema, washiriki wapatao 700 wanatarajiwa kushiriki ambao ni pamoja na Viongozi mbalimbali wanawake kutoka Barani Afrika na Nje ya Afrika katika ngazi ya Marais, Marais Wastaafu, Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu, Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa, Watu Mashuhuri, Mawaziri wanaosimamia sekta ya biashara na masuala ya jinsia na wanawake, vijana na wafanyabiashara. 

Sambamba na Kongamano hilo, kutakuwa na maonesho ya wafanyabiashara yatakayohusisha wafanyabiashara wanawake kutoka katika nchi 55 za Afrika.

Aidha amesema, kongamano hili la Wanawake katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, ni Kongamano la pili kufanyika ambapo Kongamano la Kwanza lililofanyika tarehe 12-14 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam ambalo lilihudhuriwa na washiriki wapatao 1060 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakiwemo viongozi wananwake katika ngazi mbalimbali. Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha Viongozi Wakuu Wanawake, Mawaziri, Wanawake Wajasiriamali na wadau wengine ili kujadili, kutoa maoni, ushauri na mapendekezo ya kuwezesha uandaaji wa Itifaki kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake na Vijana kushiriki kikamilifu katika biashara ndani ya AfCFTA.

Vilevile amebainisha mafanikio makubwa yaliyotokana na Kongamano la kwanza la mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kupata maazimio yaliyowezesha kuandaa na kukamilisha Rasimu ya Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara ndani ya AfCFTA ambayo kwa upande wa Tanzania iko katika hatua mbalimbali za kuridhiwa ili iannze kutumika nchini

Pamoja na kufanikiwa kwa itifaki hiyo, Kongamano hilo lilitoa njia sahihi za kutatua vikwazo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na vijana katika biashara ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara barani Afrika, ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha, taarifa za masoko, pembejeo, matumizi ya teknolojia, masoko, uwezo mdogo wa kufuata viwango na mahitaji mengine ya kisheria. Amesema Dkt. Kijaji.

Dkt Kijaji pia amesema mafanikio hayo yanajumuisha Kampuni 18 zinazofanya biashara ya kuuza bidhaa katika soko la AfCFTA yakiwemo makampuni ya wanawake ya ANISIA Group (Tanzania) linalouza bidhaa za karafuu nchini Morocco na AJA (T) Ltd linalouza Kamba za katani nchini Ghana. Makampuni haya yanatimiza lengo la Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nane (8) za mwanzo zilizopewa kipaumbele cha kupeleka bidhaa 10 zitakazotangulia kuingia katika soko hilo kuanzia Julai Mosi 2023.

Aidha, amewasisitiza wananwake kushiriki wa katika kuimarisha mnyororo wa thamani katika bidhaa, hasa kilimo na misitu na kuuza bidhaa zao kupitia soko la AfCFTA.

Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo tayari zimesharidhia Mkataba huo. Baraza la Mawaziri lilipitisha Waraka wa kuridhiwa kwa Mkataba huo tarehe 7 Agosti 2021 na Bungeni la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likapitisha rasmi Azimio la kuridhia Mkataba huo mnamo tarehe 9 Septemba 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news