Tanzania yapokea mkopo wa shilingi bilioni 32 ujenzi njia ya kusafirisha umeme Benaco hadi Kyaka

RIYADH-Tanzania imepokea mkopo wa dola milioni 13 sawa na shilingi bilioni 32 kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Saudi kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Benaco hadi Kyaka mkoani Kagera.

Mkataba wa mkopo huo umesaiiniwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko huo Bw. Sultan Almsarshad, wakati wa Mkutano wa Masuala ya Uchumi kati ya Nchi za Kiarabu na Afrika uliofanyika Riyadh- Saudi Arabia.

Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Dkt. Mwamba alisema kuwa mkataba huo wa mkopo wa shilingi bilioni 32 utawezesha ujenzi wa njia ya msongo umeme wa Kilovolti 220 yenye urefu wa kilometa 167 pamoja na kuboresha eneo la Benaco - Kyaka na kujenga kituo kipya eneo la Benaco na huduma za ushauri.

“Mradi huo chini ya mkataba tuliosaini unatekeleza Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26 na ni sehemu ya ajenda kuu ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayolenga kujenga uchumi shindani wa viwanda na vipaumbele kwa maendeleo ya watu kupitia mikakati mbalimbali,” alisema Dkt. Mwamba.

Dkt. Mwamba alisema mradi wa Kyaka- Benaco umekuwa ukitekelezwa kwa msaada wa fedha kutoka katika Muungano wa nchi zinazouza mafuta/petroli (OPEC) ambao umechangia dola milioni 60, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Umoja wa Falme za Kiarabu dola milioni 30 na Serikali ya Tanzania dola milioni 2.4.

Alisema kuwa mkopo uliosainiwa ni moja ya mikopo inayotolewa na mfuko huo katika kutekeleza miradi mbalimbali, ambapo Tanzania imenufaika na mfuko huo hasa katika sekta za maji, miundombinu ya Barabara na afya Tanzania Bara na Zanzibar.

Alisema kuwa Serikali imekusudia kuongeza na kusaidia uchumi na maendeleo ya jamii nchini kwa kuwezesha sekta ya nishati na kuwapatia watu wake shughuli mbalimbali za kufanya zinazotekelezwa na mradi huo.

Aidha aliongeza kuwa Mfuko huo utabaki kuwa mbia mkubwa kwa Tanzania katika kusaidia kukuza Maendeleo ya taifa na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Mfuko huo kuendeleza mahusiano ya maendeleo.

Mfuko wa Maendeleo wa Saudi ulianzishwa kwa lengo la kusaidia nchi za kiarabu. Hata hivyo mwaka 1974 sanjari na ongezeko kubwa la rasilimali walipanua wigo kwa kuweza kusaidia nchi zote zinazoendelea na sasa unasaidia zaidi nchi za Afrika na Asia..

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news