Serikali yatoa ufafanuzi wa mifugo iliyokamatwa Serengeti

NA HAPPINESS SHAYO

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema kuwa suala linalohusisha ng'ombe 806, kondoo 420 na mbuzi 100 waliokamatwa Serengeti na kupigwa mnada baada ya Mahakama ya Musoma kutoa hukumu, limeshahitimishwa kimahakama baada ya taratibu zote kukamilika.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Novemba 9,2023 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Ngorongoro, Mhe. Emmanuel Ole Shangai aliyeilalamikia Serikali kuhusu mifugo hiyo iliyokamatwa na Askari wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika eneo la Mugumu Serengeti na kupelekwa mahakamani kisha kupigwa mnada.

“Ni suala ambalo limehitimishwa mahakamani kupitia kesi ya jinai namba 10 ya mwaka 2023 kwa kuingiza mifugo hifadhini isivyo halali na tayari hukumu ilitolewa, na tarehe 1 Novemba 2023 ilielekezwa dalali wa mahakama ateuliwe kwa ajili ya kupiga mnada wa hadhara kwa kufuata taratibu kama ambavyo sheria yetu ya wanyamapori ya mwaka 2009 lakini vilevile sheria yetu zinazosimamia Hifadhi za Taifa zinavyoelekeza,”Mhe. Kairuki amesisitiza.

Amesema, kufuatia mnada huo kutokana na hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Musoma zilipatikana fedha kiasi cha shilingi milioni 169,264.

Aidha, ameongeza kuwa lengo la Serikali kwa mujibu wa Ibara ya 27 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria ambazo zimewekwa ni kuendelea kulinda hifadhi za Taifa pamoja, maliasili na uoto wa asili uliomo ikiwa ni pamoja na wanyama na viumbe vingine vilivyoko katika maeneo yaliyohifadhiwa

Kufuatia ufafanuzi huo, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ameipa Serikali muda wa kuliangalia upya suala hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news