Wafugaji walivyo na wajibu wa kutunza mazingira nchini

NA GODFREY NNKO

UFUGAJI wa kimkakati nchini ni miongoni mwa njia nyingine muhimu ya kuwezesha uhifadhi wa mazingira kwa ustawi wa kizazi cha sasa na kizazi kijacho.
Hii ni kwa kuzingatia ukweli kuwa, ulinzi wa mazingira ni jukumu ambalo linamuhusu kila mtu, vikundi, taasisi, mashirika, na Serikali ili kuhakikisha mazingira asilia yanaendelea kuwa endelevu.

Kwa hiyo, ni muhimu kulinda maliasili na mazingira ya sasa ya asili, na pia kurekebisha kasoro ambazo zinasababisha madhara na kubadili mwelekeo inapowezekana.

Umuhimu wa uhifadhi wa mazingira ni mkubwa, ikizingatiwa kuwa, Dunia ni makao ya aina mbalimbali za viumbe hai, na sote tunaitegemea kwa chakula, hewa, maji, na mahitaji mengine.

Kwa kuhifadhi wanyamapori na maliasili nyinginezo, maisha ya binadamu yatakuwa yenye afya na salama.

Uhifadhi unahusisha kuhifadhi aina mbalimbali za spishi, mifumo ikolojia, pamoja na huduma za kimazingira kama vile virutubisho vya nitrojeni.

Hivi karibuni, Mhadhiri kutoka Chuo cha Mipango mkoani Dodoma, Dkt.Francis Njau alikaririwa akisema kwamba, ufugaji wa kisasa ni njia moja wapo ya kutunza mazingira, lakini ufugaji huria ni chanzo cha uharibifu wa mazingira.

“Kuna aina kama tatu za ufugaji, lakini nikiziweka kwa ujumla wake ni kwamba kuna ufugaji huria ambapo ng’ombe wanaondoka wanakwenda kufugwa nje, halafu jioni wanarudi wanakaa kwenye zizi.

“Lakini, kuna ufugaji mwingine ambao tunasema nusu huria ambapo kuna wakati mfugaji anawaweka ndani na kuna wakati anawatunza nje.

“Lakini, ufugaji wa kisasa wale wana maeneo maalum, ng’ombe wanafugwa ndani saa 24, chakula wanaletewa ambako wanafugia ng’ombe wao na katika maeneo hayo unaweza ukakuta kwamba wanatunza yale malisho yao ya asili.

“Lakini wakati huo huo wanapanda malisho yao wenyewe na wanaongezea chakula hizi supplements kwa ajili ya mifugo yao, ndiyo maana mifugo yao wanakuwa wazuri kwa sababu wana uhakika wa chakula,”anafafanua Dkt.Njau.

Dkt.Njau anafafanua kuwa,kwa sasa sera zinakataza ufugaji holela kutokana na aina ya ufugaji huo kuchangia katika uharibifu mkubwa wa mazingira.

“Wafugaji wa kisasa angalau wanatunza mazingira kwa sababu utakuta kwamba wana eneo maalum la kufugia na wakati huo huo wamepangilia mashamba yao, hawatoi ng’ombe kwenda kufungia sehemu zingine, ukweli ni kwamba kwa mfano hapa Dodoma, ng’ombe mmoja anahitaji kuwa na hekta nne za malisho.

“Sasa fikiria kwamba mtu ana ng’ombe 100 ina maana inabidi awe na hekta karibu 400, sasa wafugaji hawana eneo kama hilo.

"Kwa wenzetu huko Ulaya ufugaji huria huwa hakuna, eneo la ufugaji wa ng’ombe lipo katika maeneo maalum mfano nchi kama Australia ambako nako kuna ukame kama huku.

“Lakini wafugaji wana maeneo yao maalum ya kufuga, na bei zao za mifugo ipo controlled haibadiliki badiliki kama ilivyo kwetu huku Tanzania, kwa sababu kwetu huku Tanzania unaweza kukuta mtu labda kuna eneo la heka 10, lakini ana ng’ombe zaidi ya 100.

“Sasa kipindi ambacho kunakuwa na uhaba lazima ahame akatafute eneo lingine au wakavamia eneo lingine ili kupata malisho ng’ombe wake wasife na hasa miundombinu ya maji nako kwenye mazingira yetu unakuta ni magumu,”anafafanua Dkt.Njau.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka wafugaji nchini kufanya ufugaji wa kimkakati usioharibu mazingira.
Ametoa rai hiyo Oktoba 31, 2023 wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Maonesho ya Ufugaji wenye Tija na Utunzaji wa Mazingira sanjari na kuzindua Chama cha Mazingira na Ufugaji Tija Tanzania (CHAMAUTA) katika viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Amesema kuwa, wafugaji nchini hawana budi kuwa mabalozi wazuri na kuungano mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira kwa kufanya shughuli za ufugaji wenye tija kwa maendeleo endelevu.

Aidha, Waziri Dkt. Jafo amesema kuwa ufugaji endelevu usioathiri hifadhi ya mazingira utasaidia katika kuepusha migogoro baina ya wakulima na wafugaji nchini.

“Tuepuke migogoro baina ya wakulima na wafugaji ambayo tunashuhudia ikitokea katika baadhi ya mikoa nchini husababisha kutoelewana kwa makundi haya mawili hali inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani, na tuna wajibu wa kulinda amani,” amesisitiza.

Kwa upande mwingine Dkt. Jafo amewahimiza wafugaji ambao wamepata ufadhili kutumia fursa ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabdiliko ya Tabianchi (COP 28) kushiriki kikamilifu.

Amesema kuwa, mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Novemba 28 hadi Desemba 5, 2023 utakuwa ni adhimu ya kuitangaza nchi yetu namna Tanzania inavyofanya ufugaji rafiki wa mazingira.

Hali kadhalika Waziri Jafo ametoa wito kwa CHAMAUTA kulitumia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupata uelewa kuhusu kanuni na zinazosimamia mazingira ili kuepuka shughuli zinazoharibu mazingira.

Amewataka wafugaji nchini kuunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaendelea kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuendeleza sekta ya maji.

Amesema, kupitia miradi mbalimbali Serikali imekuwa ikichimba malambo kwa ajili ya kunyweshea mifugo hususan katika maeneo yenye ukame hatua inayosaidia

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Remidius Mwema aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia utekelezaji wa uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Amesema kuwa, mikakati ya kuhifadhi vyanzo vya maji katika eneo la Makutupora inaendelea na kuwa tayari chanzo hicho kimeanza kutoa asilimia 61 ya mahitaji ya maji kwa mkoa.

Aidha, Mhe. Mwema amesema kuwa Serikali ya Mkoa inaendelea na Kampeni ya Kukijanisha Dodoma ambapo inaendelea kuandaa vitalu vya miche ili kukabiliana na upungufu wa miche.

Naye Mwenyekiti wa CHAMAUTA,Jeremiah Wambura amesema chama hicho kimemtunuku Waziri Jafo kadi ya uanachama wake na mlezi kumuomba kuwa mlezi wake kutokana mchango wake na Ofisi kwa ujumla.

Wambura amesema,lengo lao ni kuhamasisha kuwa na vyakula bora yakiwemo maziwa na utunzaji mazingira kwa manufaa ya ufugaji wa sasa na baadaye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news