Waziri Mchengera aagiza wote waliohusika kuchoma maduka moto Kariakoo wakamatwe, huenda wakahukumiwa jela maisha

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameagiza wale wote waliohusika kuchoma moto maduka ya wafanyabiashara Kariakoo wakamatwe.
Mheshimiwa Mchengerwa ametoa agizo hilo leo Novemba 15,2023 baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa ukarabati na ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

“Lakini, nichukue fursa hii kumwelekeza Mheshimiwa Mkuu wa mkoa kutokana na madhara ya moto ambayo yamekuwa yakiendelea mara kwa mara, tunatambua eneo letu karibu na hapa sokoni kulitokea madhila ya moto ambayo yaliunguza vibanda vya watu na kuhatarisha maisha ya Watanzania katika eneo hili.

“Na kusababisha hasara kubwa sana, kwanza kwa Watanzania wachuuzi ambao wanafanya biashara katika eneo hili ambao wengi walikopa fedha kwenye mabenki mbalimbali.

“Lakini, pia madhila mbalimbali yaliyotokea katika eneo hili.Nimpongeze Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu ya hatua alizochukua mara moja kuhakikisha kwamba ameunda kamati ya uchunguzi, baada ya kuunda kamati ya uchunguzi akaja kutoa taarifa ya uchunguzi walioufanya.

“Na mimi nikiri kwamba, nilikuwa ninakusubiri Mkuu wa Mkoa utoe taarifa ya uchunguzi tofauti na vile ambavyo wengi wanafahamu, wakati huo unafanya uchunguzi na mimi nilituma watu wangu kufanya uchunguzi.

“Kwa hiyo ile ripoti niliyo nayo nitakuletea, utaiunganisha na ripoti uliyo nayo wewe.Lakini, pia nikiri kwamba makosa haya ya uchomaji wa majengo ni makosa makubwa sana.

“Pengine Watanzania hawafahamu kosa la uchomaji wa jengo lolote, kosa lake ni kubwa sana.Inaweza ikampelekea aliyefanya kosa hilo kufungwa miaka 30 mpaka kifungo cha maisha jela.

“Sasa Watanzania ni lazima wajue hayo, na nichukue fursa hii kukuelekeza pamoja na kwamba ripoti ulikwishaisoma nitakuletea na ripoti ya uchunguzi ambayo timu yangu ilifanya ili uziunganishe pamoja.

“Lakini, maelekezo yangu wale wahusika wote wanafahamika kwa sababu moto huu si moto au janga ambalo pengine Mwenyenzi Mungu alilitengeneza.

“Wala si hitilafu ya moto kusema kwamba zilitokea shoti za umeme, wapo watu, kikundi cha watu ambacho kilitekeleza jambo hili.

“Kwa hiyo, maelekezo yangu wale wote waliohusika wakamatwe mara moja na wafikishwe kwenye vyombo vya sheria, wapelekwe mahakamani.

“Kwa sababu ninatambua kwamba mlifanya uchunguzi, lakini sijayasikia maelekezo yoyote kuhusu wale waliohusika.

“Sasa, maelekezo yangu wale wote waliohusika wakamatwe kwa sababu wanafahamika, waliopelekea moto huu kuzuka, kusababisha hasara, kusababisha maumivu makubwa kwa Watanzania ambao walikuwa wanafanya shughuli zao katika eneo lile basi wahusika wote wakamatwe mara moja na wafikishwe mahakamani.

“Kwa hiyo, nimekuelekeza Mkuu wa Mkoa kuhakikisha kwamba wahusika wamekamatwa na wamefikishwa mahakamani, kwa sababu wanajulikana waliofanya kitendo hiki, hayo ndiyo maelekezo yangu,”amesisitiza Mheshimiwa Mchengerwa.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Mchengerwa amesema, Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na majanga mbalimbali ya moto nchini.

“Baada ya tukio lile, nilikwishatoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa yote nchi nzima kwanza kujipanga, kuhakikisha kwamba wanadhibiti matukio ya namna hii.

“Lakini, pia yako maelekezo ya moja kwa moja ambayo tumewapatia wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya kuhakikisha kwamba tunajiandaa vizuri na majanga ya namna hii,”amesema Waziri Mchengerwa.

RC Chalamila

Wakati huo huo,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amesema, ameyapokea maelekezo ya Waziri Mchengerwa kwa utekelezaji wa haraka.

“Lakini, jambo la pili nimepokea maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, yale yote yanayohusiana na soko hili, lakini zaidi pamoja na masuala mengine yanayohusiana na pale Kariakoo Auction Mart.

“Taratibu zote, Mheshimiwa Waziri wewe ni Mwanasheria unafahamu vizuri, zote tuko katika hatua nzuri na baada ya hapo tutakupa taarifa ili uweze kuiona, kama ambavyo tunashughulika nao watu hawa.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news