Waziri Mchengerwa aridhishwa na ujenzi Soko la Kariakoo,Chalamila ataja masharti

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa ameridhisha na ukarabati na ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Ameyasema hayo leo Novemba 15,2023 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kukagua ukarabati wa Jengo la Soko Kuu la Kariakoo.

“Nichukue fursa hii kupongeza uongozi wa usimamizi wa soko hili la Kariakoo,lakini na Mwenyekiti Mama Ghasia.

“Lakini, pia nimpongeze Mkuu wa Mkoa na nikipongeze Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, kwa usimamizi mzuri wa soko hili ambalo ndiyo kitovu cha Dar es Salaam.

“Unapoizungumzia Dar es Salaam, unaizungumzia Kariakoo na Soko la Kariakoo lina historia kubwa sana.

“Lazima tumshukuru na kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha takribani shilingi bilioni 28 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu wa soko la Kariakoo ambalo ni soko lenye historia pan sana ya nchi yetu Tanzania.

“Lakini, pia unapolizungumzia Jiji la Dar es Salaam unalizungumzia Soko la Kariakoo, kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais.

“Leo tumefanya ukaguzi na nimeridhika kwamba, ujenzi unakwenda vizuri na takribani asilimia 85 imekwishatekelezwa.

“Na sisi tunaamini kabisa kwamba Mkandarasi kufikia mwezi wa pili mwakani atakuwa amemaliza na tutamuomba Mheshimiwa Rais yeye mwenyewe aje awakabidhi wananchi.

“Watanzania, wananchi wa Dar es Salaam soko hili la Kariakoo, kwa hiyo nimeridhika na ujenzi.Na ndiyo maana nachukua fursa hii kuwapongeza sana wasimamizi, nichukue fursa hii kumpongeza Mkuu wa Mkoa kwa ufuatiliaji wa karibu, kuja mara kwa mara.

“Lakini, pia kufuatilia kuhakikisha kwamba thamani ya fedha iliyotolewa na Mheshimiwa Rais inakwenda kukidhi malengo ambayo Mheshimiwa Rais ameyakusudia katika ujenzi wa soko la kisasa kabisa la Kariakoo ambalo sasa limeongezwa mara dufu, tofauti na pale lilipokuwa awali.

“Sasa hivi, kutakuwa na maduka mengi, migahawa mingi, na maeneo mengi ya uchuuzi ambayo Watanzania wataweza kuyatumia wakati wa soko hili la Kariakoo.

“Kwa hiyo, tumshukuru Mheshimiwa Rais na mimi niendelee kumuomba Mkandarasi anayetekeleza mradi huu kuhakikisha vile viwango ambavyo Serikali imevikusudia wakati anamalizia utekelezaji wa mradi huu basi kisipungue kiwango hata kimoja.

“Maana yake ni kwamba tunagegemea tupate soko la kisasa zaidi, wakati wa umaliziaji wa utekelezaji wa mradi huu.

Hawa Ghasia

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Shirika la Masoko Kariakoo, Mheshimiwa Hawa Ghasia amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kufanikisha ujenzi huo.

“Nichukue fursa hii, kwanza kumshukuru sana Mheshimiwa Rais ambaye amewezesha ujenzi huu kufikia katika hatua hii ambayo imefikia kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema.

“Mheshimiwa Rais alitoa zaidi ya shilingi bilioni 28 kwa ajili ya kukarabati lile soko ambalo lilikuwa limeungua.

“Lakini,pia kujenga soko jipya hili ambalo sasa hivi tupo, kwa hiyo tunamshukuru sana.Kwa sababu, kabla ya moto hapa kulikuwa na kisoko kidogo sana ambacho mtu akija sasa hivi kwa kweli ni mabadiliko makubwa sana.

“Pia, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuja kututembelea na kututia moyo, tuna imani kabisa zile changamoto ambazo ameziona atatusaidia katika kuzifanyia kazi.

“Kwa namna ya kipekee nimshukuru sana sana Mkuu wa Mkoa kwa sababu yeye ndiye msimamizi wa moja kwa moja wa mradi huu.

“Kwa hiyo tunamshukuru sana, sisi na yeye tuko bega kwa bega kuhakikisha kwamba mradi huu unakamilika, lakini pia tutakaa kwa pamoja na mkuu wa mkoa na tutahakikisha wale wote ambao walikuwemo ndani ya soko kabla ya kuungua moto ndiyo watakaopewa kipaumbele kurudi soko litakapokamilika.

“Baada ya maboreho haya kufanyika, wafanyabiashara wategemee mabadiliko makubwa sana. Kwamba, kwa takwimu ukiangalia mwanzo na sasa hivi wafanyabiashara wengi sana watapata nafasi ya kuingia hapa kwa sababu pamoja na kwamba tulikuwa tunasema kulikuwa na wafanyabiashara walikuwa 1,000.

“Lakini, wengi walikuwa wanapanga chini, wanafanyia biashara katika mazingira magumu,lakini sasa hivi baada ya kukamilika asilimia karibu yote watarudi, watakaa katika mazingira ya heshima, ya kisasa na ya ubora zaidi.

“Na, pia kama ambavyo mmeona katika ukarabati na ujenzi huu zile changamoto za mifumo ya kuzimia moto, mifumo ya maji taka na mifumo ya kisasa ya umeme, vyote vimezingatiwa wakati wa huu tunavyokuja.

“Kwa hiyo, tunategemea na wao pia wanavyokuja wambadilike na kama wasipobadilika, nadhani soko lenyewe litawabadilisha.”

RC Chalamila

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amesema kuwa, “Nitumiue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mchengerwa pamoja na uongozi wa soko hili chini ya Mama Ghasia.

“Kwa sababu soko hili linakwenda vizuri katika hatua zake za ujenzi, na sisi tunaendelea kumuahidi Mkandarasi kwamba tutaendelea kumlipa haraka kadri ambavyo vyanzo vya fedha vitakapokuwa vikipatikana.

“Lakini, jambo la pili nimepokea maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, yale yote yanayohusiana na soko hili.

“Lakini, jambo la tatu Mheshimiwa Waziri soko hili umeliona na linakwenda vizuri.Niwape tahadhari wananchi wote wale ambao wamekuwa wakikutana na matapeli huko na huko, kwamba soko hili wamekwishaanza kulipishwa fedha au la.

“Soko hili, hakuna hatua zozote mpaka sasa ambazo zimekwishaanzwa ambazo zinahusiana na masuala ya ulipiaji wa vyumba hivi.Mara baada ya taratibu hizo zitakapokuwa tayari tutawapeni taarifa.

“Lakini, mtakumbuka kwamba soko hili awali liliendeshwa kwa hasara sana, watu wengi walikuwa hawana mikataba.

“Moja ya masharti makubwa ya muhimu na ambayo mtu atakapoyavunja itakuwa ni kinyume kabisa cha sheria ni kuanza biashara kwenye soko hili bila kuwa na mkataba.

“Lakini, na jambo lingine la msingi ni kwamba kodi iliyokuwepo awali lazima itajadiliwa upya ili kuweza kuwa katika viwango vya soko la sasa.

“Soko ambalo linalingana na uwekezaji wa Kariakoo, lakini na jambo lingine la muhimu sana tunasema, Mheshimwa Rais alikwishaagiza kwamba soko hili lianze kufanya kazi saa 24.”

Pia, amesema suala la usalama kwa soko hilo la Kimataifa limepewa kipaumbe kikubwa kwani zitafungwa kamera za kutosha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news