ACP Morcase:Wanahabari usalama wenu unaanza na ninyi

NA FRESHA KINASA

WAANDISHI wa habari wametakiwa kuwa makini na kuchukua tahadhari za kiusalama wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao wakiwa katika maeneo hatarishi na yenye migogoro ili waendelee kuwa salama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara ACP Salim Morcase ameyasema hayo Desemba 12, 2023, Mjini Musoma wakati akizungumza katika mdahalo uliowakutanisha Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara na Jeshi la Polisi Mkoani humo.Ambapo umeandaliwa na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC).

Kamanda Morcase amesema kuwa, Wanahabari wanapaswa kutambua kuwa, usalama wao unaanza na wao wenyewe kujiandaa vyema kabla ya kwenda katika majukumu yao na kufahamu vyema maeneo wanayokwenda kutekeleza majukumu yao hasa maeneo hatarishi ili wawe salama zaidi.
Ameongeza kuwa, wanahabari pia wanalojukumu la kuwa wasikivu wanapotahadharishwa na Jeshi la Polisi wakati wa utekelezaji wa majukumu yao hasa maeneo ya maandamano na yenye hatari kubwa za kiusalama badala ya kukaidi kwani kunaweza kuhatarisha usalama wao.

Aidha,amewataka Wanahabari kuwa wazalendo ikiwemo kuangalia maudhui yasiyofaa katikaJamii kwani yanaweza kuleta taharuki na kuondoa usalama na amani katika Jamii.
Huku akisema kuwa anathamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari Katika kuibua masuala mbalimbali na kuiamsha mamlaka kuchukua tahadhari.

"Vyombo vya habari vinawajibu mkubwa katika kutanzua uhalifu kwa kutoa taarifa na kuelimisha umma kuhusu matukio ya uhalifu jinsi yanavyotendeka na kuchukua tahadhari dhidi ya matukio hayo.
"Sisi Jeshi la Polisi tunavitumia kutoa elimu mbalimbali kwa jamii jinsi ya namna uhalifu unavyotendeka na jinsi ya kuchukua tahadhari ya uhalifu huo na kwa kiasi kikubwa tumepata mafanikio makubwa hasa ya kupunguza uhalifu hao mkoani Mara," amesema Kamanda Morcase.
Pia amewaomba waandishi wa habari mkoani Mara kuendelea kuwa na ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu pamoja na kutii sheria bila shurti ili kuondokana na migongano ambayo inaweza kuwatia hatiani.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara, Raphael Okello amesema kuwa mdahalo huo ni muhimu kwani utaweza kuimarisha mahusiano mazuri baina ya wanahabari mkoani humo na Jeshi hilo katika utendaji wa kazi.

Aidha, Okello amewataka Waandishi wa Habari Mkoani humo kuendelea kuandika mazuri ya Mkoa wa Mara ili kuleta taswira nzuri ya mkoa huo kitaifa na Kimataifa.
Naye Edmund Kipungu kutoka UTPC amesema, kuwa, lengo la kuendesha midahalo hiyo ni kutaka kuondoa changamoto ambazo zimekuwepo baina ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news