DCEA: Matumizi ya dawa za kulevya huchangia kuongezeka maambukizi ya VVU

NA DIRAMAKINI

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA), Aretas Lyimo amesema,matumizi ya dawa za kulevya huchangia kuongezeka kwa maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU).

Ameyasema hayo Desemba Mosi, 2023 katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Morogoro mkoani Morogoro.

Kupitia maadhimisho hayo ambayo yaliongozwa na kauli mbiu ya “Jamii Iongoze Kutokomeza UKIMWI”, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, DCEA ni wadau muhimu katika kuhakikisha Taifa linatokomeza dawa za kulevya na maambukizi ya VVU.

“Sisi Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ni wadau wakubwa wa Siku ya UKIMWI Duniani kutokana na UKIMWI na dawa za kulevya vinashabihiana kwa kiasi kikubwa kutokana na kutumia sindano hususani wale wanaojidunga.

“Lakini pia kutokana na matumizi ya dawa za kulevya wale wanaofanya ngono zembe na wao huwa wanaathirika zaidi na UKIMWI.

“Hivyo, sisi mamlaka ni wadau wakubwa katika siku ya leo, lakini pia katika wiki hii ya UKIMWI tumefungua pia Kituo chetu cha MAT Kliniki ambacho kitakuwa kinahudumia warahibu wa dawa za kulevya hapa Morogoro,na viunga vyake na kituo hicho kimejengwa katika Gereza la Kihonda na Waziri Mkuu wetu Kassim Majiliwa Majaliwa kupitia kwa Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan aliomba na tukapata fedha hiyo na tukajenga kituo kikubwa cha kisasa kabisa ambacho kitahudumia watu wote wale wa Morogoro ambao ni warahibu na kutoka viunga vyake.

“Kwa hiyo, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga kituo hicho kikubwa ambacho kitahudumia warahibu ili waweze kurudi katika hali zao za kawaida na waweze kulijenga Taifa letu na waweze kutimiza malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kujenga Taifa lenye uchumi endelevu,”amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo kwa mwaka huu alikuwa ni Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu kupitia kilele hicho cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani alizindua Ripoti ya Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI ambayo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua nchini.

Ni kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Waziri Mkuu alisema, hiyo ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume.

Alisema, Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na UKIMWI ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Utafiti huo unaotambulika kama Utafiti wa Viashiria vya UKIMWI kwa mwaka 2022/2023 unapima matokeo ya mwitikio wa kitaifa wa UKIMWI nchini miongoni mwa watu wazima wenye umri wa kuanzia miaka 15 ukiwa na lengo la kukadiria kiwango cha maambukizi mapya ya VVU.

Sambamba na ushamiri wa VVU, ufubazaji wa VVU kwa watu wanaoishi na VVU na utumiaji wa dawa kitaifa na kimikoa.

Kuhusu DCEA

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.

Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.

Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news