Dira hii itasaidia Taifa kupanga mipango yake-Rais Dkt.Samia

DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameainisha changamoto zinazopaswa kupewa kipaumbele ikiwemo kufungamanisha ukuaji wa uchumi na sekta za uzalishaji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akibonyeza Kitufe kuashiria uzinduzi wa Mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wananchi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Rais Dkt.Samia amesema hayo kwenye maadhimisho ya miaka 62 ya Uhuru wa Tanzania Bara sanjari na Mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.

Aidha, Rais Samia ametaka sekta mbalimbali za uzalishaji ziimarishwe zaidi ikiwemo kilimo ambayo inakua kwa asilimia 4 tu kwa sasa tofauti na inavyotakiwa.

Pia amesisitiza kuimarishwa kwa ushiriki wa sekta binafsi ndani na nje ya nchi ili kufanya wenyeji kuwa na utayari wa kupokea na kushirikiana na wageni wanaokuja kuwekeza na kufanya biashara nchini.

Rais Samia amesema dira hiyo mpya itatakiwa kuzingatia kigezo cha kuongeza pato la kila mwananchi kufikia dola za Kimarekani 3,000 kwa mwaka ambacho hakikufikiwa katika dira ya mwaka 2000-2025.

Amesema, kushindwa huko kulisababishwa na ukuaji wa uchumi kutojielekeza kwenye sekta zinazogusa maisha ya watu wengi, hivyo umasikini vijijini haujapungua kwa kasi iliyotarajiwa.

Kuhusu suala la Maadili ya Taifa, Rais Samia amesema ni muhimu taifa kuwa na watu mahiri, makini na waadilifu ili kupata jamii inayochukia rushwa kila mahali, inayojituma na kufanya kazi bila kusukumwa na inayopinga na kulaani ukwepaji kodi.

Vile vile, Rais Samia ametoa wito kwa Watanzania wote ndani na nje ya nchi (Diaspora) kushiriki kutoa maoni katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo kupitia njia za kisasa zitakazoainishwa na Tume ya Mipango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news