Hazina Saccos yatoa msaada wa viti mwendo Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH)

NA ASIA SINGANO
WF

CHAMA cha Ushirika cha Akiba na Mikopo Hazina ‘Hazina Saccos’ kimetoa msaada wa viti mwendo 15 kwa Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH) vyenye thamani ya sh. milioni tano kwa ajili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hazina Saccoss Bw. Afrikar Tonono (kushoto), akikabidhi viti mwendo 15 kwa Kaimu Mkurugenzi Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Kessy Shija, ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii. Makabidhiano hayo yamefanyika hospitalini hapo jijini Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Bw. Festo Mwaipaja, alisema lengo la kutoa viti hivyo ni kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuboredha huduma za afya nchini.

“Sisi kama Hazina Saccos tumetoa viti mwendo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuzingatia mahitaji muhimu katika jamii, viti hivi vitasaidia wazee wasio na uwezo wa kutembea au wagonjwa waliozidiwa ili waweze kufikishwa maeneo ya utoaji huduma kwa urahisi maana hayati Mwalimu Julias Nyerere alipambana na ujinga, maradhi na umasikini,” alisema Bw. Mwaipaja.
Uongozi wa Hazina Saccos ukiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, baada ya kuhitimisha zoezi la kukabidhi viti mwendo 15 kwa Hospitali hiyo jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma).

Alisisitiza kuwa Chama hicho kimeona umuhimu wa kusaidia Hospitali hiyo ambayo imekuwa ikitoa huduma nyingi za kibingwa kwa wananchi wa Kanda ya Kati.

Bw. Mwaipaja alitoa wito kwa watumishi wa umma nchini kujiunga na Saccos hiyo huku akisisitiza kuwa wataendelea kuhudumia jamii inayowazunguka kwa kutoa misaada mbalimbali muhimu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Kessy Shija, aliishukuru Hazina Saccos kwa kutoa msaada huo wa viti mwendo huku akieleza kuwa uhitaji wake bado ni mkubwa.

“Viti hivi vinahitajika sana, mahitaji ni makubwa maana hii ni Hospitali ya Kanda na inatoa huduma nyingi za kibingwa na inatibu magonjwa makubwa, wazee wanatumia viti kwenda maeneo mbalimbali kupata huduma wanapofika hapa’’, alisema Dk. Shija.

Alisema Hospitali hiyo kwa sasa inahudumia wagonjwa 800 kwa siku na kwamba licha ya uwepo wa viti hivyo ni vichache na mahitaji yamekuwa yakiongezeka ambapo hadi jana vimefika 75 hivyo wanahitaji vingine kama 100.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news