Kamanda Mallya amfutia leseni dereva aliyezidisha abiria, makondakta wakamatwa Songwe

SONGWE-Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi, ACP Theopista Mallya ameendelea na operesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria kwenye barabara ya kwenda Mbeya-Tunduma katika kituo cha ukaguzi wa magari Mahenje wilayani Mbozi.
Katika operesheni hiyo ya Desemba 30, 2023 kamanda Mallya alimfutia leseni dereva Ally Lugenge (56) akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili T855 DXL Kampuni ya Masihi inayofanya safari zake Ubaruku-Mbeya-Tunduma na Ileje.

Gari hilo aina ya Fuso yenye uwezo wa kubeba abiria 45,kondakta na dereva wa gari hilo walipakia abiria zaidi ya 66 pamoja na mizigo kitu ambacho ni kinyume na taratibu za sheria za usalama barabarani pia ni hatari kwa usalama wa abiria.

Kamanda Mallya alichukua uamuzi wa kumfutia leseni dereva huyo baada ya kurudia kosa la kuzidisha abiria ambapo alipewa onyo kali kisha kutozwa faini, lakini dereva huyo alirudia kosa lile lile ambalo lilimpelekea Kamanda Mallya kumfutia leseni dereva huyo.

Sambamba na hilo, Kamanda Mallya aliwakamata makondakta wawili wa mabasi madogo ya abiria kwa kosa la kuchanganya abiria na mizigo kwenye gari la abiria ambalo ni kosa kwa sheria za usalama barabarani, makondakta hao ni Frank Dicksoni (24) pamoja na Zakayo Msimwa (21).

Aidha, Kamanda Mallya alitoa wito kwa madereva na makondakta kufuata sheria za usalama barabarani bila shuruti pia aliwataka abiria kujisimamia wenyewe pindi waonapo gari limejaa wanatakiwa wasipande na sio mpaka wamuone askari ndio watii sheria za usalama barabarani.

Kamanda Mallya amesema,kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake ili kupunguza ajali ambazo zinaepukika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news