Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu:Serikali yazindua Barabara ya Dunga-Zuze

ZANZIBAR-Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Mh. Hamza Hassan Juma amewataka wananchi kuendelea kuzienzi na kuzitunza barabara zinazojengwa karibu na maeneo yao ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Ameyasema hayo huko Dunga-Zuze katika uzinduzi wa Barabara ya kilomita 1.85 ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Aidha, amewataka wananchi kuacha kujenga pembezoni mwa barabara ili kujikinga na ajali zinazoweza kueupukika.

"Nawaomba wananchi muache kujenga pembezoni mwa barabara na pia mnatakiwa muzingatie na kuheshimu mipaka iliyowekwa katika barabara," alifahamisha Waziri.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa barabara hiyo umewarahisishia wananchi ikiwemo wakulima kupeleka bidhaa zao kutoka vijijini kwenda mjini.

Waziri Hamza amesema, lengo la Mapinduzi ni kuendeleza kwa vitendo mambo mazuri yaliyoachwa na Hayati Mzee Abeid Amani Karume ili wananchi waondokane na unyonge uliyokuwepo kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964.

Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Nane chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kujenga barabara zote kwa kiwango cha lami Mjini na Vijijini.

Hata hivyo ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kazi kubwa waliyoifanya pamoja na wananchi kwa kuwa wastahamilivu katika kipindi chote cha ujenzi wa Barabara hiyo.

Akitoa taarifa ya kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Khadija Khamis Rajab amesema jumla ya Tsh. milioni 80 zimetumika katika ujenzi huo hadi kukamilika kwake.

Aidha amebainisha kuwa Barabara hiyo ya kiwango cha lami imejengwa na Kampuni ya IRIS kutoka Uturuki na ujenzi ulianza Novemba 22 na kukamilika Desemba 2, mwaka huu.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Ayoub Moh'd Mahmoud amesema, mkoa umedhamiria kusheherekea Mapinduzi kwa vitendo kwa kushirikiana na viongozi wenzake.

Nao wananchi wa Dunga na maeneo ya jirani wameipongeza Serikali kwa kuwajengea barabara hiyo kwani itawasaidia kusafirisha bidhaa zao sambamba na kuwaondoshea usumbufu waliokuwa wanaupata kwa muda mrefu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news