Mvua zaathiri mamia ya nyumba Geita

GEITA-Nyumba 556 za makazi ya watu katika Tarafa ya Kasamwa ndani ya Halmashauri ya Mji wa Geita mkoani Geita zimepata madhara kufuatia mvua zilizonyesha zikiambatana na upepo kuanzia Oktoba 18, 2023 hadi Novemba 10, 2023.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa Maafa wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Valeria Makonda katika hafla ya ugawaji wa msaada kwa waathirika wa mafuriko ndani ya halmashauri hiyo.

Amesema, Mkoa wa Geita tayari umepokea tani 22.1 za mahindi pamoja na vifaa vya msaada wa kibinadamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kaya ambazo makazi yao yaliharibiwa na mvua ikiwemo za Halmashauri ya Mji wa Geita.

Pia,amebainisha miongoni mwa wanufaika wa msaada wa mahindi hayo ni waathirika wa nyumba hizo za makazi zilizoharibiwa na mvua, ambapo waathirika wamepatiwa msaada wa vyakula na malazi vilivyotolewa na Serikali.

Katika taarifa yake kwa Mkuu wa wilaya Mratibu huyo wa Maafa ameeleza kuwa, mpaka sasa kiasi cha shilingi milioni 225.46 kinahitajika ili kukarabati miundombinu ya taasisi za umma zilizoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe akizungumza baada ya kugawa vifaa vya kibinadamu, amewataka waathirika wa mvua hizo kutumia vyema misaada waliyopewa na serikali na kuwaelekeza watendaji kufuatilia misaada hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news