Mwinjilisti Temba atoa tiba msongamano wa malori Dar

NA DIRAMAKINI

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonse Temba ameishauri Serikali kuzifunga yadi zote zilizopo jijini Dar es Salaam huku akisisitiza umuhimu wa kupata yadi maeneo ya Maili Moja mpaka Chalinze kwa ajili ya kuegesha malori.

Temba ambaye ana uzoefu wa kufanya huduma na kushuhudia uendeshaji wa huduma za usafiri katika mataifa zaidi ya 10 duniani amesema, changamoto ya kujaa malori mjini haina faida kwa jamii na Taifa.

"Tatizo kubwa lingine ninaloliona nchini ukilinganisha na mataifa mengine 12 niliyotembelea ambalo ni hatari mno ni ujaaji wa malori mjini.

"Tunatambua kuwa, bado malori hao yanachukua mizigo bandarini kwa sasa na bandari kavu ya Kwala bado haijaanza kutoa mizigo mingi.

"Lakini, hili halisababishi Jiji la Dar es Salaam kuwa dampo la malori hasa pembezoni mwa barabara zikiwemo zile za dharura mfano Barabara ya Ubungo kwenda Buguruni hasa eneo la Mwananchi limegeuka gereji, oil chafu inamwagika lami inaharibika huku kilomita moja ya ujenzi ni zaidi ya shilingi bilioni moja.

"Ushauri wangu, si kuyazuia malori Kibanda cha Mkaa Mbezi bali wenye malori kutafuta yadi Maili Moja na Chalinze kwa ajili ya kuegesha malori yao kwa wingi na kuruhusu machache kwenda bandarini moja kwa moja kuchukua mizigo.

"Fungeni yadi zote zilizoko Dar es Salaam, toeni vibali hata kwa sasa 48, hata kwa laki tatu au chini ya hapo. Ikumbukwe malori mengi yanatoka nchi jirani ambapo mara nyingi huwa kuna milipuko ya magonjwa kama kipindupindu, homa, ebola na mengineyo.

"Hivyo, hayo yanaweza kuambukiza wananchi, kwani malori hayo yamekuwa yakioshwa kila kona ya Dar es Salaam kiholela, hivi karibuni lori la mafuta lilipata ajali juu ya Daraja la Mfugale nusura lianguke likazuiwa na kingo za ukuta."
Mwinjilisti Temba amesema, endapo lori hilo lingeanguka lingesababisha mlipuko mkubwa wa moto na vifo vingetokea.

"Ajali kama hii pia iliwahi kutokea Magari Saba Mbezi, ajali ile mbaya iliuwa watu wengi kwa mlipuko wa moto. Hatuombi kujirudia, yapo mengi tunaomba TANRODS msikae ofisini huku Watanzania wanateketea.

"Mna jukumu la kusaidia kupanga mji na kuondoa mirundikano ya foleni jijini, pia Tunduma inahita upanuzi wa barabara, watu wanateseka sana,"amefafanua Mwinjilisti Temba.
Wakati huo huo, Mwinjilisti Temba amesema kuwa, tatizo la ajali katika barabara ya Morogoro halipaswi kufumbiwa macho kwani lina madhara makubwa kwa jamii na Taifa.

"Kuanzia Mlandizi hadi Morogoro kumekuwa na mfululizo wa ajali kila mara na kusababisha kwa wiki mbili zaidi ya magari saba na kuendelea kupata ajali, hivyo watu kupoteza viungo vya mwili na wengine kufariki.

"Ajali hizi ambazo zinaambatana na wizi wa mizigo katika magari pamoja na kuwaibia wageni mbalimbali, wanaofanya hivyo ni vijana wajulikanao kwa jila la 'shushashusha' wanaokimbiza magari hususani ya mizigo na kuiba.

"Baadhi ya taarifa huwa hazitolewi polisi kwa sababu ya wageni kutokuwa na msaada wa kufanya hivyo. Haya yote yanatokea barabara ya Morogoro ambayo imezidiwa sana na wingi wa magari, hivyo pale madereva wanapopata upenyo wakipata ajali hukimbia.

"Najua kuwa, Serikali ipo mbioni kutafuta mkandarasi wa ujenzi wa barabara kupitia PPP, lakini hata barabara hiyo ikianza mwezi wa tano 2024, ujenzi utachukua muda mrefu hadi kukamilika pengine 2030 ambapo itakuwa Watanzania wengi wamekufa na kupata ulemavu kwa ajali zilizoko kila kukicha."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Hongera sana Mheshimiwa Temba kwa hoja na michango mizuri katika kulijenga Taifa letu, kwa muda mrefu nimekuwa nikikufuatilia kupitia maandiko yako Diramakini hakika yanatupa nuru na mwanga. Mfano kuhusu hili suala la msongamano wa malori mjini umeshauri vema, ninaamini mamlaka husika zitachukua hatua hili si tu kudhibiti ajali bali kuokoa fedha nyingi ambazo Serikali yetu huwa inapoteza kutokana na foleni hizo.. Asante

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news