Mwinjilisti Temba:Rais Dkt.Samia ni dira ya Watanzania

NA DIRAMAKINI

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonse Temba amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha demokrasia, amani, umoja na mshikamano nchini huku akisema ni dira sahihi ya Watanzania.
Temba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio Penuel mkoani Kilimanjaro amesema, uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia umeendelea kufanya mambo mengi mazuri ambayo licha ya kulifanya Taifa kustawi kiuchumi pia wawekezaji kutoka ndani na nje wanaendelea kuhamasika kuja kuwekeza mitaji yao hapa nchini.

Ameyasema hayo Desemba 2,2023 baada ya kushiriki na wadau mbalimbali kwenye matembezi ya kilomita tano ya amani na maridhiano ambayo yaliratibiwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT). Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa.

"Nimefurahi sana leo kwa JMAT kutuunganisha pamoja na Serikali, katika matembezi haya ya kumuunga mkono Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

"Mtanzania mwingine anaweza kuona kama hivi ni vitu vya kawaida sana, hivi vitu si vya kawaida kwa sababu ni maono kwa ajili ya Tanzania, nataka niwaambie Watanzania wenzangu kwamba, katika nchi zote za Afrika na duniani hakuna nchi yenye maono mazuri kama haya ya matembezi ya amani.

"Katika kutembea, na mimi nimebahatika kutembea na Waziri Mkuu karibu kilomita kilomita tano, katika kutembea na Waziri Mkuu nimeshuhudia wazi kabisa, wananchi, wageni mbalimbali ambao tulikuwa tunapishana nao barabarani iwe Waazungu, Watanzania wenzetu wengine wanafurahi, yaani wanashangilia kabisa wanaonesha hamasa.

"Watu wanakuwa na mshangao ni nini hiki, na bahati nzuri nimepata muda wa kuongea na Waziri Mkuu nikamuomba mwakani matembezi haya kupitia JMAT yafanyike Mkoa wa Kilimanjaro, akatoa maagizo kwa Katibu Mkuu na Mwenyekitti kwamba mwakani 2024 matembezi ya kuiunga mkono Serikali na kazi za Mama yetu Samia Suluhu Hassan yafanyike."

"Mimi nimeona leo maono ya Mwalimu Nyerere na Karume yanaendelea kuishi kwa sababu baada ya uhuru walitengeneza amani na fursa mbalimbali na ndizo Watanzania tunaendelea kupokezana vijiti na leo Rais wetu Samia Sulu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amefanya jambo nzuri sana kwa sababu ya maono yale, kama vile Waziri Mkuu alivyosema ameendelea kudumisha amani na demokrasia nchini."

Aidha, wakati akizungumza na washiriki wa matembezi hayo katika Ukumbi wa Karemjee jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwataka viongozi wa dini waendelee kusisitiza amani miongoni mwa waumini wao.

“Viongozi wa madhehebu ya dini endeleeni kuwahimiza waumini wenu kulinda amani ya nchi yetu. Wafahamisheni waumini athari za kutozingatia thamani ya amani tuliyonayo huku mkisisitiza wajibu wa kila mmoja kuhakikisha amani inadumishwa hapa nchini,”alisema.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Askofu Israel ole Gabriel Maasa alisem,a jumuiya hiyo ina matawi kwenye mikoa yote 26 ya Tanzania Bara na kwenye wilaya zake.

Akielezea mambo waliyofanikiwa kuyafanya hadi sasa, Askofu Maasa alisema: “Tumeongoza zoezi la uchangiaji damu katika baadhi ya hospitali nchini, tumefanya zoezi la upandaji miti, tumeshirikiana na Serikali kupinga unyanyasaji kwa watoto na wanawake, tumepinga ukatili dhidi ya wanaume na kuongoza mafunzo ya uraia kwa wananchi ili waipende na kuijali nchi yao.”

Akitoa salamu kwa niaba ya Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Ally Khamisi Ngeruko alisema: “Mufti na Sheikh Mkuu Dkt. Abubakar Zubeir bin Ally alisema, "Tanzania imejaa amani lakini Watanzania wanajipangaje kutumia fursa mbalimbali kwa kutumia amani tuliyonayo.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news