OSHA:Lengo letu ni kulinda uwekezaji wa rasilimali watu

NA GODFREY NNKO

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema, wakala huo unafanya kazi ili kulinda uwekezaji wa rasilimali watu ambayo Serikali imewekeza nchini.

Ameyasema hayo leo Desemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri wa vyombo vya habari nchini na wanahabari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Serikali ilikaa ikaona hapana, lazima kuwe na chombo ambacho kama huyu mtu ataingia kwenye ajira lazima ijue anafanya kazi katika mazingira gani.

"Wakakaa wakatengeneza chombo kinachoitwa OSHA ili kisimamie mazingira ya kazi na kumlinda mfanyakazi.Tunafanya kaguzi ili kulinda uwekezaji wa rasilimali watu ambayo Serikali imewekeza,"amesema.

Mwenda amesema, OSHA ni wakala wa Serikali iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu). Wakala huo ulianzishwa Agosti 31, 2001 kama sehemu ya mpango wa maboresho ya kutoa huduma kwa wananchi.

"Wengine tutakumbuka kulikuwa na zile programu za reforms, ndizo ambazo zilitengeneza OSHA baada ya kufanya tathimini na kuona kwamba, kuna haja ya usimamizi wa watu kujitegemea ili visibility yake iweze kuonekana."

Kwa mujibu wa kifungu Na. 16 cha Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, wamiliki au wasimamizi wa sehemu zote za kazi nchini wanapaswa kuhakikisha kwamba maeneo husika ya kazi yanasajiliwa na OSHA ili kuiwezesha taasisi kuwafikia kwa ajili ya kuwapa huduma nyinginezo za masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.

"Ndiyo maana OSHA ikaanzishwa chini ya Sheria za Wakala Na.30 ya mwaka 1997 kama Sehemu ya Mpango wa Maboresho ya Huduma za Serikali kwa Umma."

Amesema, kabla ya OSHA kulikuwa na sheria ambapo, hii ilikuwa ni kitengo ndani ya Idara ya Kazi ambacho kilikuwa kinajulikana kama Kitengo cha Ukaguzi wa Viwanda.

OSHA hufanya ukaguzi mbalimbali katika sehemu za kazi ili kuhakikisha kwamba kunakuwa na mifumo madhubuti ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwa ajili ya kulinda nguvukazi dhidi ya ajali, magonjwa, vifo vinavyoweza kusababishwa na mazingira ya kazi yasiyo rafiki.

"Ndiyo maana mpaka sasa hivi kuna baadhi ya watu wanadhani OSHA ipo kwa ajili ya viwanda tu, lakini kabla ya OSHA hii tuliyo nayo leo ilikuwa ni kitengo ndani ya Idara ya Kazi.

"Ilikuwa inajulikana kama Kitengo cha Ukaguzi wa Viwanda na kilikuwa kinatekeleza majukumu yake kupitia Sheria Na.297 ya mwaka 1950, ndiyo ambayo ilikuwa inasimamia masuala ya usalama na afya."

Mwenda amesema, kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia, mabadiliko ya kisiasa, mabadiliko ya kiuchumi, utandawazi na masuala mengine ya maendeleo Serikali iliamua kufanya maboresho, kwani Sheria ya mwaka 1950 ilijikita zaidi katika kusimamia masuala ya usalama.

"Ni masuala ya usalama tu na masuala ya afya hayakuzingatiwa katika ile sheria, lakini vile vile sheria ile ilijikita katika maeneo ya viwanda tu, kwa hiyo maeneo mengine yote ya kazi yalikuwa hayaangaliwi na tunafahamu kwamba hakuna maeneo ambayo ni salama katika kufanya kazi.

"Kwa hiyo ikapelekea sasa ile sheria iweze kurejewa, lakini sheria ile haikuangalia ubora wa huduma zinazotolewa ambazo zingeweza kumlinda mfanyakazi kama ambavyo nimesema kwamba, mfanyakazi ni uwekezaji wa Sertikali.

"Lakini, masuala ya usalama na afya ni masuala ya kujenga utamaduni,na ili ujenge utamaduni unahitaji uongeze uelewa kwa hiyo, masuala ya kuwa na programu za kujenga uelewa haikuwa sehemu ya ile sheria kwa hiyo baada ya kufanya tathimini, ikaonekana kwamba ile sheria inabidi irejewe.

"Ili iweze kukidhi vitu vyote hivyo viweze kuwa nyenzo ya kumlinda mfanyakazi. Lakini, Tanzania ni nchi mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani na katika shirika lile kama mwanachama kuna misingi ambayo tunatakiwa kuifuata na msingi mmoja wapo ni msingi wa masuala ya usalama na afya.

"Maana ya kuwa na chombo mahususi cha kusimamia usalama na afya, kwa kuwa hakikuwa chombo ilikuwa haikidhi matakwa yake ya Shirika la Kazi Duniani ambapo mkataba Na.155 na Mkataba Na.187 unahitaji kila nchi mwanachama kuwa na chombo mahususi cha kusimamia masuala ya usalama wa afya.

"Kwa mantiki hiyo utakuta kwamba, sasa kusudi la kuanzishwa chombo hiki (OSHA) ilikuwa ni lazima kuwe na chombo ambacho kitaboresha ustawi wa wafanyakazi kwa kusimamia usalama na afya mahala pa kazi kupitia Sheria Na.5 ya mwaka 2003."

Mwenda amesema, lengo ni kuhakikisha kwamba, maeneo ya kazi yanaweka mifumo ya kudhibiti athari za viatarishi sehemu za kazi ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokea mahali pa kazi.

"Na hatimaye hapo sasa tunalinda nguvu kazi za Taifa, na kwa kufanya hivyo maana yake tunatengeneza uwepo wa ajira zenye staha na kwa kuhakikisha kwamba usalama wa watu upo, usalama wa watu na uwekezaji upo, lakini tunaongeza ufanisi.

"Na tukiongeza ufanisi sehemu zetu za kazi, maana yake ni kwamba tunakuza pato la Taifa. Kwa hiyo ninaomba tutambue hilo kwamba, jukumu kubwa la taasisi yetu ni kuhakikisha maeneo ya kazi yanaweka mifumo ya kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokea sehemu za kazi.

"Ili kulinda nguvu kazi, kulinda mitaji, lakini vile vile kuhakikisha wafanyakazi wanazalisha kwa tija ili tuweze kukuza pato la Taifa, hiyo ndiyo OSHA,"amesema Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA.

Uchunguzi wa afya za wafanyakazi ambao hutekelezwa na wakaguzi wa afya wa OSHA hufanyika katika hatua tatu muhimu ambazo ni kabla ya kuanza kazi, mfanyakazi akiwa kazini na mfanyakazi anapoachana na mwajiri wake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu, kuacha kazi, kuondolewa kazini.

Jambo hili hufanyika ili kutambua endapo afya ya mfanyakazi inamuwezesha kumuda majukumu anayokabidhiwa na mwajiri wake pamoja na kutambua endapo mfanyakazi amepata athari zozote kutokana na mazingira ya kazi yasiyo rafiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news