PBPA yajivunia mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita uhakika wa mafuta nchini

NA GODFREY NNKO

WAKALA wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umesema, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nishati ya mafuta inapatikana wakati wote na kwa bei nafuu.

Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA) ulianzishwa mwaka 2015 kwa Amri ya Serikali (Establishment Order,2015) chini ya Mwongozo wa Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agencies Act, (Cap.245) kwa lengo la kuratibu na kusimamia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja.

Sambamba na kuhakikisha ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi ili kupata manufaa ya kiuchumi na upatikanaji wa mafuta nchini wakati wote.

Mtendaji Mkuu wa PBPA, Erasto Mulokozi ameyabainisha hayo leo Desemba 11,2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Katika kutekeleza hilo amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imetoa ruzuku kwenye gharama ya mafuta kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai 2022 hadi Desemba 2022 ili kupunguza bei ya mafuta kwa wananchi iwe stahimilivu.

“Hii ilifanyika baada ya athari ya bei ya mafuta kupanda sana katika soko la dunia kutokana na vita baina ya Urusi na Ukraine.”

Pia, amesema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imekuwa ikitoa kiasi fulani cha dola za Marekani kwa benki za biashara ili ziweze kulipia mafuta yanayotumika nchini.

Mulokozi amesema, Serikali kupitia Benki Kuu ilibadilisha baadhi ya miongozo ya udhibiti wa dola za Marekani ili kuwezesha benki za biashara kupata fedha hizo kutoka sokoni.

Vile vile amefafanua kuwa, Serikali kupitia PBPA ilibadilisha mikataba ya uagizaji mafuta na kuruhusu matumizi ya fedha nyingine za kigeni katika ulipiaji mafuta yaliyoagizwa kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi.

Aidha, amefafanua kuwa, Serikali kwa kupitia taasisi wadau imefanya mapitio ya nyaraka mbalimbali zinazosimamia Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ili kuimarisha usimamizi wa sekta ndogo ya mafuta.

“Serikali kupitia mamlaka zake imekuwa ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maghala ya kuhifadhia mafuta ili kuhakikisha taratibu za uendeshaji wa maghala hayo zinazingatiwa.

“Na imewezesha ushirikiano mzuri baina ya taasisi wadau katika sekta ya mafuta ili kuboresha ufanisi wa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja.”

Bw.Mulokozi amezitaja taasisi hizo kuwa ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na PBPA.

Katika hatua nyingine, Mulokozi amebainisha kuwa, Serikali imekuwa ikipokea maoni ya wabunge na kuyafanyia kazi katika kuboresha Mfumo wa BPS.

Mulokozi akizungumzia kuhusiana na kuanzishwa kwa Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Bulk Procurement System - BPS) amesema,Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 iliekeleza kuwa mafuta yote yatakayotumika nchini lazima manunuzi yake yafanyike kwa ufanisi.

Aidha, sheria hiyo imeweka hiari kwa mafuta ya transit kutumia mfumo huu au njia nyingine binafsi. “Hata hivyo kutokana na ufanisi mzuri wa mfumo zaidi ya asilimia 95 ya mafuta ya transit huagizwa kupitia BPS.

“Ili kuhakikisha kwamba ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini iliandaa Kanuni za Kusimamia Ununuzi wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum (Bulk Procurement) Regulation-2011).

"BPS ni mfumo wa usimamizi wa uagizaji wa bidhaa za mafuta ya petroli kwa pamoja (Bulk Importation).”.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Yasin Sadick ameipongeza mamlaka hiyo kwa kazi nzuri inayofanya kwa maslahi makubwa ya Taifa.

"Wengi wetu tulidhani PBPA ni kikundi cha Waarabu ambacho kimejikusanya na kuagiza mafuta hivyo kuiuzia Serikali, kumbe ni taasisi ya Serikali, hongereni sana kwa kazi nzuri."

Aidha, ametoa wito kwa mamlaka hiyo kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari na wanahabari ili waweze kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu majukumu yanayofanywa na mamlaka hiyo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news