Salamu za Jumapili:Mwenendo wako na Mungu

NA LWAGA MWAMBANDE

NI wazi kuwa, bila uhusiano wa kawaida na Mungu, basi umuhimu wa kumwamini Mungu unapotea katika maisha yako.
Tambua,kuunda uhusiano wa kawaida na Mungu kunapatikana kikamilifu kupitia kuutuliza moyo wako mbele zake.

Uhusiano wa kawaida na Mungu unamaanisha kuweza kutoshuku au kukataa kazi yoyote ya Mungu na kutii, na zaidi ya hayo unamaanisha kuwa na nia sahihi mbele ya Mungu, sio kufikiria kujihusu, daima kuwa na maslahi ya familia ya Mungu kama jambo muhimu zaidi haijalishi kile unachofanya, kukubali kutazamiwa na Mungu, na kukubali mipangilio ya Mungu.

Aidha, una uwezo wa kuutuliza moyo wako mbele za Mungu kila unapofanya chochote, hata kama huelewi mapenzi ya Mungu, bado ni lazima utimize wajibu na majukumu yako kadri ya uwezo wako.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,mwenendo wako na Mungu upo mikononi mwa Bwana. Endelea;

1. Katika maisha yetu, mengi tunayapitia,
Mengine mazuri kwetu, na mengine tunalia,
Yawe mema au butu, Mungu atuangalia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

2. Mashujaa wa imani, vema kuwaangalia,
Livyoishi duniani, hadi mwisho kufikia,
Changamoto si amani, ambazo walipitia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

3. Hata wewe nami pia, moyo tusijezimia,
Wakati tunapitia, changamoto za dunia,
Mungu anaangalia, yetu ametupimia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

4. Unakatishwa tamaa, imaniyo shikilia,
Magonjwa yakuvagaa, kwake Mungu angalia,
Usijekukaakaa, jina la Yesu itia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

5. Yusufu tumwangalie, njia aliyopitia,
Nduguze wamchukie, na kutaka mfagia,
Watake wamfukie, utumwa kumpatia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

6. Kwa Portifa kufikia, alidhani katulia,
Mara mke amjia, ataka kumwingilia,
Pamoja na kukimbia, gerezani aishia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

7. Kwa vile mwenendo wake, Mungu aliujulia,
Hata kwa kufungwa kwake, kibali lijipatia,
Kwa yule mkuu wake, jela akitumikia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

8. Zile ndoto kufasili, wale liwasaidia,
Walipopata kibali, maisha kuyarudia,
Walimwacha hana hali, mle ndani ajutia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

9. Farao kuota ndoto, ndiko kulisaidia,
Jela akapata wito, ikulu akaingia,
Ni Mungu wala si lotto, ndoto kumtegulia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

10. Mara njaa kuingia, katika ile dunia,
Nduguze kamfikia, chakula kufwatilia,
Yeye nani kumwambia, hofu ikawaingia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

11. Angelitaka lipiza, vile walimfanyia,
Ili nao kuwakwaza, aweze kufurahia,
Ila aliwatuliza, maneno kuwaambia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

12. Mungu alinipeleka, mbele kuwatangulia,
Shida hii kuwafika, chakula wahifadhia,
Nanyi muweze okoka, wokovu wa kuzidia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

13. Yusufu alitambua, yale aliyopitia,
Mungu yote alijua, wapi atakoishia,
Wala hakujisumbua, yale walimfanyia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

14. Daudi naye sikia, mafuta mmiminia,
Ufalme kuingia, ikulu hakuingia,
Porini alirudia, kondoo kujichungia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

15. Njia aliyopitia, angeweza kufulia,
Vitani akaingia, Goliati jipigia,
Watu walifurahia, Sauli akachukia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

16. Kilichofwata kuwindwa, ili aweze ishia,
Ila na Mungu lilindwa, Yonathani kuingia,
Mtesi wake kashindwa, ikulu akaingia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

17. Ndivyo kwa wewe na mimi, maisha tunapitia,
Kama geji haisomi, tusibaki tunalia,
Huo wote ni uvumi, tusije tukatitia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

18. Unaona wachukiwa, hapo unapofanyia,
Kiwingu unatiliwa, hapo uweze salia,
Wala usijepaliwa, imani kuachilia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

19. Ndivyo unaandaliwa, ni ngazi pa kupandia,
Wala hautachelewa, kibali kitakujia,
Kutaisha kuonewa, uweze kufurahia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

20. Changamoto zikifika, ya Yusufu angalia,
Mashambulizi wachoka, ya Daudi angalia,
Na yakupe kutosheka, Mungu akuangalia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

21. Vita vitoke kusini, wewe ulipo tulia,
Viwe vya kaskazini, yupo akupigania,
Pande zote duniani, huwezi ukaishia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

22. Mungu wetu twakuomba, sisi twakushangilia,
Mara nyingi tukiomba, wewe unatusikia,
Kwetu unabaki mwamba, yote tunayopitia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

23. Na kumbe maisha yetu, wewe watuangalia,
Hata changamoto zetu, zote unazijulia,
Ni matayarisho kwetu, nafasi kuzifikia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

24. Utusaidie Bwana, imani kushikilia,
Dhambi zinapotubana, tuweze kukurudia,
Mema tupate yaona, hadi tutapoishia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.

25. Kushukuru tukumbushe, yote tunayopitia,
Ili nawe uzidishe, sisi kutusaidia,
Mabaya yote yapishe, kwako tukifurahia,
Mwenendo wako na wangu, u mikononi mwa Bwana.
(Mithali 20:24, Mwanzo 45:7-8, 1 Wathesalonike 5:18)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news