TUGHE yasisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wafanyakazi sehemu za kazi

ARUSHA-Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimewasisitiza waajiri nchini kuimarisha dhana ya ushirikishwaji kati ya uongozi na wafanyakazi ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kujenga mahusiano mazuri kazini.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Cde.Hery Mkunda wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 29 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) kilichofanyika Ijumaa, tarehe 22 Desemba 2023 jijini Arusha.

Akielezea umuhimu wa Mabaraza ya Wafanyakazi, Cde. Mkunda ameeleza kuwa, Mabaraza ya Wafanyakazi hutoa nafasi kwa Wafanyakazi kuwasilisha maoni yao katika uongozi na kushauriana namna bora ya kuboresha utendaji wa taasisi.

Hivyo, amewaomba waajiri wote kufanya vikao vya Mabaraza ya Wafanyakazi kwa mujibu wa sheria inavyowataka kufanya vikao viwili kwa mwaka ikiwa ni vikao vya kupanga bajeti na kingine cha ufuatiliaji wa utekelezaji wa mipango hiyo.
Aidha,ametoa rai kwa wafanyakazi wote nchini kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kuwa na sauti ya pamoja katika kusimamia maslahi yao na kuwataka waajiri kuacha kuwachagulia wafanyakazi wao vyama vya kujiunga na badala yake wawachie uhuru wa kuchagua chama cha kujiunga kulingana na sekta wanayotoka.
Akifungua kikao hicho cha 29 cha Baraza la Wafanyakazi wa RITA mgeni rasmi, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Pindi Chana (MB) amewapongeza RITA na TUGHE kwa kuwa na mwendelezo mzuri wa kufanya vikao hivyo na kuutaka uongozi kuchukua maoni kutoka kwa wafanyakazi na wadau mbalimbali ya namna bora ya kuboresha utendaji wa taasisi yao.

Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa RITA, Bw. Frank Kanyusi amemshukuru mgeni rasmi kwa kuja kufungua kikao hicho cha Baraza hilo kitakachofanyika kwa siku mbili huku jumla ya wajumbe 53 wakishiriki pamoja na kuwasilishwa kwa mada mbalimbali.
Awali akiwasilisha risala ya wafanyakazi kwa Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la RITA, Bw. Adam Mkolabigawa pamoja na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuendelea kuboresha maslahi ya Wafanyakazi pia ameiomba Serikali kushughulikia na kutafuta muafaka wa suala la “kikokotoo” kwa watumishi wa umma.

Ni kama ambavyo iliahidiwa na Mheshmiwa Rais ili kupata muafaka mpya tofauti na hali iliyopo sasa ya kikokotoo cha asilimia thelathini na tatu (33%).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news