VICOBA havijafutwa,vipo 48,000 kwa sasa nchini-BoT

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa,Village Community Banks (VICOBA) hazijafutwa kwani mpaka sasa zilizosajiliwa zinafikia 48,000 nchini na usajili unaendelea.

Hayo yamesemwa na Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Deogratias Mnyamani wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya madai ya kufutwa kwa Village Community Banks (VICOBA) kupitia mahojiano na Efm Redio ya jijini Dar es Salaam.

Mnyamani alikuwa anatoa ufafanuzi kuhusu taarifa hizo za upotoshaji ambazo zilisambaa awali zikidai kuwa VICOBA vimefutwa nchini, badala yake wanachama wangepaswa kujiunga kupitia CMG.

“VICOBA havijafutwa,” amesema taarifa ambazo zilitolewa awali kuhusu kufutwa kwa VICOBA hazikutolewa na Benki Kuu.

“Ni kweli taarifa hii imeleta taharuki, lakini niseme tu kwamba, taarifa hii haikutolewa na Benki Kuu ambayo ndiyo mamlaka, taarifa hizi zilitolewa na taasisi nyingine ambazo hatutahitaji kuzizungumzia hapa.

“Niseme kwa kuanzia taarifa hii inahitaji kuwekwa sawa, hii taarifa kama ilivyotoka haikuwa sawa inahitaji kuwekwa sawa na usawa ni upi?.

“Nilisema wakati wa kujibu swali la mwenzetu Mpoki alivyozungumzia lile daraja la nne, daraja la nne linaitwa Vikundi vya Kijamii vya Huduma ndogo za Fedha kwa Kiingereza inaitwa Community Microfinance Groups (CMG).

“Sasa CMG imeweka nini ndani yake, kwenye kapu la CMG moja ya vitu vilivyopo kuna kitu kinaitwa VICOBA na ndiyo vililipa umaarufu, tuna VICOBA rasmi vilivyosajiliwa zaidi ya 48,000 nchi nzima na bado usajili unaendelea.

“Ikifika labda mwezi wa sita mwakani tunaweza kufika 80,000 hata laki moja,kwa hiyo VICOBA ni vitu rasmi vipo katika kapu la Microfinance Community Groups, kwa hiyo naomba wasikilizaji (Watanzania) wapate hiyo meseji very clear,VICOBA havijafutwa, VICOBA vinarasimishwa. Sheria inataka VICOBA virasimishwe,”amefafanua Mnyamani.

VICOBA ni mfumo wa kuweka na kukopa kwa wanachama waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi.

Mfumo huu ulianza Tanzania miaka kadhaa iliyopita na umeonesha mafanikio makubwa kwa wanachama wake kuweza kukopeshana, kusaidiana katika matatizo mbalimbali, kuanzisha miradi ya pamoja ya kiuchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news