Wataalam wa Radiolojia wapata mafunzo ya usalama wa mionzi

ARUSHA-Zaidi ya wataalam 80 wanaotoa huduma kwa kutumia vyanzo vya mionzi kwa ajili ya uchunguzi na tiba kutoka hospitali mbalimbali hapa nchini wanashiriki katika mafunzo ya Kitaifa ya Usalama wa Mionzi yanayoendeshwa na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kanda ya kaskazini jijini Arusha.
Mafunzo haya yaliyoanza leo Jumatatu tarehe 11 Desemba 2023 yatafanyika kwa muda wa siku tano.

Mafunzo haya hufanyika kila mwaka ili kuongeza ufanisi wa kazi kwa wataalamu wa radilojia katika kuhakikisha huduma ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali kwa kutumia mionzi inaendelea kutolewa kwa umakini mkubwa ili kulinda wagonjwa na wafanyakazi dhidi ya madhara ya mionzi.
Akifungua mafunzo hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Mkuu wa idara ya huduma za ufundi na kinga ya mionzi ya TAEC, Bw. Yesaya Sungita amewataka washiriki hao kuhakikisha wanapata uelewa mzuri katika mafunzo hayo ili yawasaidie katika kuhakikisha wanalinda afya za watanzania ili wasipate madhara yatokanayo na mionzi.

Bw. Sungita amesema kuwa lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwaongezea washiriki ufanisi ili kuboresha utendaji kazi na hatimaye waweze kujikinga wanapokuwa wanatoa huduma hiyo kwa kuwalinda wagonjwa na wananchi dhidi ya madhara ya mionzi kwa kutoa dozi ambayo ni sahihi kwa kufuata sheria za usalama wa mionzi mahala pa kazi bila kusahau kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa inayoelekeza namna bora na salama ya matumizi sahihi ya mionzi.
Mbali na matumizi ya mionzi katika sekta ya afya, mionzi pia inatumika katika maeneo mbalimbali kama vile kwenye viwanda, migodini, sehemu za utafiti, ujenzi wa miundombinu, kilimo na mifugo, hivyo TAEC itaendelea kutoa mafunzo ya namna hii ili kuendelea kuwajengea uwezo wataalamu katika kuendelea kutoa huduma ambayo ni salama na hatimaye kuendelea kuwalinda watanzania dhidi ya madhara ya alisema Bw. Sungita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news