Askari mwingine akamatwa na dawa za kulevya Manyara

MANYARA-Jeshi la Polisi mkoani Manyara linamshikilia Askari wa Usalama Barabarani kutoka mkoani Arusha, SGT Ismael Katenya (48) kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.

Ni dawa za kulevya aina ya mirungi mabunda 340 yenye uzito wa kilo 140 aliyokua ameweka ndani ya mabegi.
Kupitia taarifa ya Polisi Manyara iliyotolewa Januari 23,204 imeeleza,askari huyo amekamatwa na askari waliokuwa doria katika Kijiji cha Silaloda Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.

Askari huyo alikuwa akitumia gari lake aina ya Nissan Patrol (T148 CTB) kusafirisha dawa hizo mkoani humo.

Kamanda wa Polisi mkoani Manyara ACP George Katabazi amethibitisha kukamatwa kwa askari huyo pamoja na gari lake.

Amesema kuwa, kwa sasa anashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini wahusika wengine wa mtandao huo wa biashara haramu huku taratibu nyingine za kisheria zikifuata.

Hayo yanajiri ikiwa ni miezi kadhaa imepita tangu Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara kumshikilia askari polisi, Mrakibu Msaidizi wa Kituo cha Polisi wilayani Arumeru mkoani Arusha, John Shauri kwa kosa la kusafirisha shehena ya dawa za kulevya aina ya mirungi gunia nne yenye bunda kilo 264.

Askari polisi huyo alikamatiwa jijini Arusha baada ya kufanikiwa kuwakimbia polisi katika kizuizi cha ukaguzi cha Minjingu mkoani Manyara Julai 14, 2023.

Kukamatwa kwa askari huyo kulithibitishwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara,Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, ACP Lucas Mwakatundu na kusema kuwa askari huyo alikamatwa Julai 16,2023 jijini Arusha.

Kamanda Mwakatundu alisema kuwa,baada ya kukamatwa alipelekwa Makao Makuu ya Polisi Babati na kusweka rumande ili aweze kujibu shitaka linalomkabili ndani ya jeshi hilo kabla ya kupata maelekezo mengine kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo.

‘’Ni kweli askari Shauri anashikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma hizo na yuko rumande akisubiri taratibu za Kipolisi ndani ya Jeshi hilo kabla ya maelekezo mengine kutoka kwa viongozi wa juu wa jeshi hilo,’’alisema Mwakatundu wakati huo.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Manyara zilisema kuwa askari Shauri aliyekuwa akiendesha gari aina ya Noah Vox rangi nyeusi yenye namba za usajili T465CUS ilikamatwa majira ya ya saa 2.30 asubuhi akiwa na shehena hiyo ya mirungi ikiwa imejaa kwenye gari hiyo.

Awali askari huyo alisimamishwa na kikosi cha doria cha Polisi Babati na kikosi hicho kilikuwa kikiongozwa na operesheni ofisa wa Polisi Babati Mrakibu Msaidizi baada ya kupata taarifa fiche kutoka kwa raia wema juu kusafirisha mara kwa mara kwa mirungi hiyo kunakofanywa na askari huyo asiye na weledi kutoka Arusha kwenda Babati.

Vyanzo vya habari vya polisi Babati viliendelea kusema kuwa, askari Shauri alikuwa akifanya biashara hiyo haramu ya kusafirisha mirungi akiwa na sare za jeshi la polisi ili iwe njia rahisi yeye kupita katika vizuizi mbalimbali vya polisi Makuyuni,Minjingu na Babati.

Habari zaidi zilisema kuwa, alipofika katika kizuizi cha Minjingu alisimamishwa na askari na aliposogelewa ili kufanyiwa ukaguzi aliondoa gari kwa kasi na kukimbia ndipo hatua ya kulikimbiza gari hilo ilipoamuriwa na Mkuu wa Operesheini Babati.

Vyanzo vya Kipolisi Babati vilisema kuwa, baada ya kukimbizwa na kufikiwa kwa karibu ili aweze kuzuiwa na crusser ya polisi,askari Shauri alipaki gari pembeni na kulitelekeza gari hilo na kutokomea msituni kusikojulikana.

Vyanzo viliendelea kusema kuwa, baada ya hatua hiyo ya askari Shauri kutokomea kusikojulikana,Mkuu wa Operesheni Babati akiwa na askari wengine kwa kushirikianana raia wema waliokwenda katika tukio hilo walipekua gari hiyo na kukuta sare kadhaa za Jeshi la Polisi,Kitambulisho cha Polisi,Kadi za Benki mbalimbali ,vitambulisho vya NIDA,Tume ya Uchaguzi,Bima ya Afya na ikabainika kuwa askari huyo ni wa Kituo cha Polisi Arumeru mkoani Arusha.

Baada ya upekuzi huo kumalizika garui hiyo ilivutwa na break down hadi Kituo Kikuu cha Polisi Babati na kukabidhiwa kwa Kamanda wa Lolisi Mkoa wa Manyara kwa hatua zaidi.

Hata hivyo, habari zaidi kutoka Polisi Babati na Arusha zilisema kuwa askari Shauri ambaye alikuwa katika mafunzo ya utimamu wa mwili katika Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoani Arusha (FFU) chini ya Mrakibu Mwandamizi,CCP Mikidadi Galilima ambaye ndiye msimamizi Mkuu wa Mafunzo hayo aliombwa ruhusa siku hiyo majira ya saa 11.30 alfajiri Julai 14,2023 na askari huyo kuwa anaumwa na alipewa mapumziko siku hiyo bila kupewa hati ya matibabu.

Vyanzo vilisema kuwa, baada ya kupewa ruhusa hiyo ndipo safari ya kuanza kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi ilipoanza kutoa Arusha kwenda Babati.

Baadhi ya askari Polisi mkoani Arusha na Manyara walisema kuwa, kuendelea kwa matukio ya uhalifu kwa askari wakubwa wa jeshi hilo katika mikoa hiyo ni kutokana na baadhi ya hatua stahiki kutochukuliwa kwa baadhi yao, kwani kuna matukio mengine kadhaa yamefanyika Arusha hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa.(LNM)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news