Dkt.Mpango:Vijana msitumike kisiasa

KIGOMA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka vijana kutokukubali kutumika kisiasa katika kuchochea vurugu, uhasama na maandamano yasiyo na tija kwa taifa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. Dkt. Philip Mpango akikabidhiwa tuzo na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mohammed Ali Kawaida iliyotolewa na UVCCM kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tuzo hiyo imetolewa wakati wa Kongamano la UVCCM kuelekea Miaka Mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani na Miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi lililofanyika Uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma leo Januari 28, 2024.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Kongamano la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kuelekea Miaka Mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan madarakani na Miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi lililofanyika Uwanja wa Kawawa mkoani Kigoma.

Amesema, uchumi wa dunia nzima umeathiriwa na UVIKO - 19, vita baina ya mataifa pamoja athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo uimarishaji wake sio suala la muda mfupi.

Amewasihi vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea maslahi ya Taifa pamoja na kutumia ushawishi wao kuwahimiza vijana wengine na watu wazima kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kuwaonesha mafanikio makubwa yaliyofikiwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Makamu wa Rais amewataka UVCCM kuendelea kuungana na kushikamana ili kujenga Jumuiya iliyo bora na yenye nguvu. Amesema UVCCM kama zilivyo Jumuiya nyingine za Chama ni muhimu katika kukiimarisha Chama hivyo ni lazima ibaki katika umoja wake kwa kuepuka kutengeneza makundi, majungu, matamko ya vitisho na kauli zisizofaa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewasihi Vijana kutambua adhma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga demokrasia na kuimarisha utawala unaojali maslahi ya watu ili kujenga ustahimilivu kwa kuepuka migongano, kutafuta suluhu na mapatano pale kunapotokea kutoelewana, kuleta mageuzi yatakayochochea kukua na kushamiri kwa nchi pamoja na kujenga na kuimarisha mifumo mbalimbali katika nchi.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa vijana kuuthamini na kuulinda kwa nguvu zote Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kukemea baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakitoa kauli zenye mwelekeo wa kubeza mafanikio ya Muungano huo. Pia amewataka Vijana wa CCM kuwa kielelezo cha uadilifu, kufanyakazi kwa bidii na kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi, mila na desturi.

Makamu wa Rais ametoa rai kwa UVCCM na vijana wote nchini kutumia mitandao ya kijamii vizuri ili kujipatia maarifa. Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa ya maendeleo ya TEHAMA kushiriki mijadala yenye tija inayolenga kutafuta ufumbuzi wa matatizo katika jamii.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amewataka vijana kushiriki katika shughuli za uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amaesema suala hilo ni pamoja na kushiriki kikamilifu katika kupanda na kutunza miti na kusaidia kudhibiti vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto hovyo. Aidha amewataka Vijana kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya nishati mbadala ya kupikia ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yameendelea kuwa makubwa na kusababisha upotevu mkubwa wa misitu nchini.

Katika Kongamano hilo mafanikio mbalimbali ya Serikali ya Awamu ya Sita yameanishwa yakiwemo katika sekta za Afya, Kilimo, Maji, Elimu, Nishati na Miundombinu. Pia UVCCM wamkabidhi tuzo ya mafanikio kwa Rais pamoja na fedha kwaajili ya kumwezesha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea Urais mwaka 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Vijana wanatakiwa kishiriki siasa. Hizi kauli za kutumika ni kauli za uchawi. Hakuna binadamu anatumika duniani. Mtu ambaye ana akili timamu anafanya jambo kwa maamuzi yake.

    Wanasiasa ambao hawapendi vijana kufanikiwa kisiasa wanatumia kauli kama hizi. Hii kauli inaonekana ya maana lakini lengo lililopo no ovu.

    Imagine kuna chama inahusisha watoto ambao wako under 18 katika siasa. Na hawaoni kama hii ni kuwatumia kisiasa. Ila kwa vijana wanaona ndio wanatumika.

    Kisheria mtoto wa chini ya miaka 18 hana uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Ndio maana mtu akimshwishi Binti au mwanafunzi mwenye umri chini ya miaka 18 inaweza kutafsiriwa kama ubakaji.

    Kama ushiriki wa watoto kwenye siasa sio kuwatumia kisiasa, vipi kuhusu vijana wenye maamuzi yao? Kuna mtu mzima anatumika?

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news